SERIKALI YATOA BILIONI 1.4/- KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KATA YA DUTUMI HUKO KIBAHA VIJIJINI

NA ROTARY HAULE

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa jumla ya sh.bilioni 1.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Dutumi iliyopo Kibaha Vijijini mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa Kamati za Huduma ya Jamii na Diwani wa Viti Maalum Kibaha Vijijini, Josephine Gunda (kushoto) akigawa kadi za UWT kwa wanachama.

Taarifa juu ya fedha hizo imewasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum, Josephine Gunda katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini uliofanyika juzi Mjini Mlandizi.

Gunda alisema kuwa, Serikali imetoa fedha hizo na zimeelekezwa katika miradi ya afya,elimu, barabara,maji na mahitaji mengine muhimu kwa wakazi wa Kata hiyo.

Alisema kuwa,kati ya hizo sh.milioni 290 zimeelekezwa kujenga upya Shule ya Msingi Kimaramisale na milioni 100 zitatumika kujenga madarasa matano katika Shule nyingine mbalimbali zilizopo ndani ya Kata hiyo.

Gunda, alisema kuwa sh.milioni 680 zitatumika katika kujenga barabara ya kutoka Mondo - Kimaramisale kwa kiwango cha Changarawe huku milioni 22 zitatumika kukarabati zahanati ya Dutumi na Kimaramisale.

Aidha,Gunda aliongeza kuwa milioni 360 zitatumika kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji ya bomba ambayo yatatoka mto Ruvu na kwamba kukamilika kwa mradi huo itawaondolea adha ya maji wakazi wa Kata hiyo.

Gunda, ameishukuru Serikali pamoja na Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kutaka kuwakomboa wananchi wa Kata hiyo huku akiwaomba wananchi na wanaCCM kuendelea kumuunga mkono Rais Samia.

"Sisi wanaKibaha Vijijini tunaishukuru Serikali na tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuitazama Kata yetu ya Dutumi kwakuwa tunaamini kukamilika kwa miradi hiyo itakuwa chachu ya maendeleo ndani ya Kata na hata Halmashauri yetu ya Kibaha Vijijini," alisema Gunda.

Gunda,alisema Kata ya Dutumi kwa sasa inaongozwa na diwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lakini Serikali ya CCM imejitoa katika kuleta maendeleo kwa wananchi wote bila ya upendeleo wa vyama na kwamba ni vyema wananchi wakasoma harama za nyakati kwa kuhakikisha wanaiunga mkono CCM.

Katika hatua nyingine Gunda,alitumia nafasi yake kutoa kadi 200 kwa Wanawake wa UWT waliopo Kibaha Vijijini ikiwa ni sehemu ya kutekeleza aadi yake aliyoitoa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno,aliwasisitiza viongozi wa CCM kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha hizo ili ziweze kutekeleza kwa wakati miradi iliyokusudiwa.

Maneno, alisema kuwa Rais Samia amekuwa akifanyakazi kubwa ya kuwapigania wananchi wake ili wapate maendeleo ndio maana anapeleka fedha nyingi katika miradi kwahiyo lazima wanaCCM washikamane katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri.

"Nadhani tunaona jinsi ambavyo Rais wetu anavyojituma na kupambana kwa ajili ya wananchi kwahiyo nawaomba na sisi wanaCCM lazima tujitoe kumsaidia Rais kusimamia fedha hizi ili kusudi aweze kutekeleza yale aliyokusudia lakini itasaidia kukiimarisha chama chetu,"alisema Maneno.

Hata hivyo,Maneno alisema mtu yeyote atakayegundulika kutumia fedha hizo vibaya au kushindwa kusimamia mradi kikamilifu lazima achukuliwe hatua kwakuwa mtu kama huyo hana nia njema na Taifa .

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news