Tanzania yapiga hatua kudhibiti maambukizi ya VVU

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Serikali imepiga hatua kubwa katika kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mujibu wa kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 hadi asilimia 83 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,Jenista Mhagama ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Novemba 14,2021 jijini Dodoma kuelekea Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani Desemba 1, 2021.

Waziri Mhagama ameeleza kuwa, kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilima 61 ya makisio ya watu wanaoishi na VVU (WAVIU) mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019.

“Serikali kupitia uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU na UKIMWI nchini,” amesema Waziri Mhagama.

Amefafanua kuwa, matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARV) kwa WAVIU wanaojua hali zao za maambukizi yameongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi asilimia 98 mwaka 2019 na kiwango cha kufubaza VVU kwa wale wanaotumia ARV kimeongezeka kutoka asilimia 87 mwaka 2016 hadi asilimia 92 mwaka 2019.

Pia ameeleza kuwa vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa 50% kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020.wakati takwimu za kiwango cha maambukizi katika jamii (HIV prevalence) zinaonyesha kiwango kilishuka kutoka 7% mwaka 2003/04 hadi 4.7% manamo mwaka 2016/17.

Mhagama amefafanua kuwa Maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) nchini Tanzania yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020. Wakati Maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (Mother to child transmission) yameshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.

Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka huu 2021 amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika kitaifa Jijini Mbeya kuanzia Novemba 24 hadi Disemba 1, 2021 katika Uwanja wa Luanda Nzovwe ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.Ameongeza kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutoa fursa ya kutathimini hali halisi na mwelekeo wa kudhibiti Virusi va UKIMWI (VVU) na UKIMWI kitaifa na kimataia, kutafakari na kutekeleza kauli mbiu inayotolewa kila mwaka kulingana vipaumbele vya kidunia kwa muktadha wa kitaifa, pamoja na kuwakumbuka watu wote waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI.

“Katika wiki ya maadhimisho hayo kutakuwa na matembezi ya hisani kwa ajili ya kutangaza na kuhamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund – ATF) ambayo yatafanyika tarehe 24 Novemba, 2021 Mbeya. Pia kutakuwa na kongamano la kisayansi kwa ajili ya kutathmini hali na mwelekeo wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini,” amesema

Sambamba na hayo alieleza kuwa kutakuwa na Kongamano ambalo litahusisha mawasilisho ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI nchini na kutakuwa na mdahalo wa vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kativilivyopo Mkoani Mbeya ambapo watajadiliana masuala mbalimbali yanayo husiana na afua za VVU na UKIMWI kwa vijana, mafanikio yaliyofikiwa vyuoni katika kukabiliana na changamoto hizo. Pamoja na hayo ameongeza kuwa kutakuwa na Mdahalo wa Viongozi wa Dini na Viongozi wa Jadi (Machifu), utakaohudhuriwa na vijana na jamii kwa ujumla

Aidha, Waziri Mhagama ameagiza wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia utekelezaji wa shughuli za maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani katika mikoa yao kwa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU na UKIMWI walioko katika Mikoa husika.

Pia ametumia fursa hiyo kuwahimiza Wakazi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani watumie fursa ya maonesha hayo kupata elimu ya afya,ushauri nasaha,upimaji wa hiari wa VVU , Upimaji wa Saratani ya Shingo ya Kizazi, Sukari, Uwiano wa Urefu na Uzito wa Mwili.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Mwenyekiti wa Baaza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bi Leticia Kapela wakati akitoa pongezi kwa Serikali jinsi inavyowajali watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko ameshukuru Serikali kwa kuendelea kupambana na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA),Leticia Kapela amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita namna inavyoendelea kuwajali watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na mikakati iliyojiwekea katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambayo yameleta mafanikio makubwa na maambukizi kupungua.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutujali sisi watu tunaoishi na virusi vya UKIMWI na sisi Baraza tutahakikisha tunashirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI,” amesema Mwenyekiti huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news