Wavamia eneo la Kanisa la Orthodox

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAMACHINGA ambao ni wafanyabiashara ndogo ndogo waliopo eneo la Mbuyuni Kata ya Wazo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam wamevamia eneo la Kanisa la Orthodox na kuanza kufanya biashara jambo ambalo limelalamikiwa na uongozi wa kanisa hilo.
Inakadiriwa kuwa, kundi la wamachinga  200 wamevamia eneo hilo la kanisa wakidai kuwa ni la wazi na linamilikiwa na Serikali hivyo, wanaenda hapo kufanya biashara zao baada ya kufukuzwa barabarani.

Makamu wa Askofu wa kanisa hilo Jimbo la Dar es Salaam, Cleophace Bachuba amesema kuvamia kwa wamachinga hao katika eneo lao kumesababisha baadhi ya shughuli za kanisa kusimama.

Amesema, tayari wameshatoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya mtaa na wilaya ambao uliwarudishia majibu kuwa hilo sio eneo la wafanyabiashara, hivyo wavamizi wanapaswa kuondoka kupisha shughuli za kanisa kuendelea.
“Wakati Serikali inafanya operesheni ya kuwaondoa wamachinga barabarani ndipo hawa wa eneo la Mbuyuni wakavamia eneo letu hili la kanisa na kukwamisha shughuli zingine kuweza kuendelea.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopanga wamachinga ili wakae vizuri ili wajipatie riziki zao, sisi wote ni jamii moja ya watanzania, kwa upande wetu tunafanya kazi na wananchi hatupaswi kugombana, kuchukiana wala kusali kwa shida, hivyo tunaomba serikali itusaidie katika hili,”amesema. 

Paroko wa kanisa hilo, Padri Frumentios Msuri amesema, kanisa hilo la Bikiria Maria lilijengwa mwaka 1939 na tangu hapo watanzania, Wagiriki na watu wa aina mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusali, lakini baada ya vurugu hizo wamelazimika kusali Upanga jijini Ilala.

“Tangu lililopojengwa tumekuwepo hapa licha ya eneo letu kumegwamegwa, leo na hawa machinga wanataka kuvamia, tunaomba Serikali ituangalie na iwapangie eneo la kwenda ndugu zetu hawa ambao wanatafuta riziki kwa ajili ya familia zao,” amesema. 

Mwenyekiti wa wamachinga hao, Kizito Ponsiano amesema, wafanyabishara hao hawafanyi biashara zao katika eneo la kanisa na kusisitiza kuwa eneo hilo sio lote ni mali ya kanisa.  

Amesema, wanauomba uongozi wa kanisa hilo kuwapatia vielelezo vinavyoonesha kuwa eneo hilo ni mali yao na kwamba wakiviona na kujiridhisha wataondoka na kutafuta eneo lingine.

Akijibu madai hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbuyuni Salasala, Robart Masawe amesema katika eneo lake wafanyabiashara wamepangiwa eneo la Benako ambalo lina mgogoro na eneo la Kisanga ambalo halina choo kwa sasa.

“Diwani anapambana sasa hivi ili kupatikane choo, tukimaliza kujenga wamachinga hawa watatolewa na kwenda kupangwa katika eneo hilo wala hakuna tatizo,” amesema

Post a Comment

0 Comments