Uwanja wa Ndege Musoma kukamilika mwakani, Mhandisi Kasekenya atoa siku saba kwa TEMESA

NA MWANDISHI MAALUM

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma utakamilika mwakani, hivyo wakazi wa Mkoa wa Mara wajipange vizuri kunufaika na fursa zote za ujenzi na matumizi ya uwanja huo.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Gofrey Kasekenya (katikati), eneo la uwanja wa ndege wa Musoma ambao ujenzi wake unaendelea alipokagua maendeleo ya ujenzi huo na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule. (Picha zote na WUU).

Akikagua upanuzi na ujenzi wa uwanja huo kwa kiwango cha lami, Mhandisi Kasekenya amesema lengo la Serikali kurefusha uwanja huo na kuujenga kwa viwango vya kisasa ni kuwezesha ndege kubwa kutua na hivyo kuufungua Mkoa wa Mara kwa kuongeza tija katika utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Kiwanja hiki kitakapokamilika kitakuwa na urefu wa mita 1,705 na upana wa mita 30 na hivyo kuwezesha ndege nyingi kukitumia na hivyo kuvutia watalii wanaokwenda Serengeti,”amesema Mhandisi Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemtaka mkandarasi anayejenga uwanja huo Beijing Construction Engineering Group (BCEG), kuzingatia ubora na kukamilisha kazi kwa wakati.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Gofrey Kasekenya (katikati), akisisitiza jambo alipokagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma ambao ujenzi wake unaendelea, kulia ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule na kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe.
Muonekano wa uwanja wa ndege wa Musoma ambao upanuzi wake wa kuuwezesha kuwa na urefu wa mita 1,705 na upana wa mita 30 unaendelea.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema zaidi ya shilingi bilioni 3, za fidia zimeshalipwa na hivyo watahakikisha ujenzi unakuwa wa viwango na unakamilika kama ilivyopangwa.

“Tumejipanga vizuri kupitia msimamizi wa maradi huu (TECU),kuhakikisha mradi unakamilika mapema na kwa viwango vya kimkataba hivyo tunawaomba wananchi watupe ushirikiano," amesisitiza Mhandisi Maribe.
Meneja wa Eakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vitalis Bilaul akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Gofrey Kasekenya alipokagua kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Mwigobero na Kinesi mkoani Mara.
Muonekano wa barabara ya Bulamba-Kisorya (KM 51), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisorya-Nansio (KM 121.9), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Mara.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya ametoa siku saba kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Mara kukutana na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo ili kupitia upya gharama za ujenzi wa jengo la kupumzikia abiria katika eneo la Mwigobero-Musoma ambazo ameelezea kutokuridhishwa nazo.

Amesema, hakubaliani na kiasi cha shilingi milioni 86, zilizopangwa kutumika kwani ni kubwa kuliko matarajio ya jengo na eneo husika.

Aidha, amemwagiza Meneja wa TEMESA mkoa wa Mara, Mhandisi Vitalis Bilaul kuhakikisha changamoto za kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma kati ya Mwigobero na Kinesi zinapatiwa ufumbuzi haraka ili kupunguza adha za usafiri kwa wananchi hususan kipindi cha mvua.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya siku mbili kukagua miradi ya ujenzi katika mkoa wa Mara.

Post a Comment

0 Comments