Wahamasishwa kuwekeza katika vyakula vyenye virutubisho

NA HADIJA BAGASHA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuwekeza kwenye sekta ya uchakataji na usindikaji wa vyakula vyenye virutubishO (lishe) ili kupunguza kiwango cha watu wenye utapia mlo.

Kauli hiyo inakuja kufuatia baadhi ya mikoa nchini ambayo inazalisha chakula kwa wingi kuwa na ongezeko la watoto wenye lishe duni ikiwemo mikoa ya Njombe, Rukwa, Ruvuma, Iringa, Songwe na Kigoma huku mkoa wa Tanga ukiwa ni mkoa ambao awali ulikuwa chini kwa asilimia 23 kwa mwaka 2014, lakini kwa miaka ya hivi karibuni mkoa huo umekuwa na takwimu zinazoongezeka hadi asilimia 34.
Waziri ameyasema hayo Novemba 18, 2021 wakati wa uzinduzi wa mpango jumuishi wa awamu ya pili mkutano wa saba wa kutathimini mpango huo wa kitaifa wa wadau wa masuala ya lishe nchini ambapo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wawekezaji kujikita katika sekta hiyo ya utengenezaji wa vyakula vyenye virutubisho.

Waziri Majaliwa amezindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Lishe wa Kitaifa wa miaka mitano (NMNAP II) na kutoa wito kwa watafiti kuanzisha tafiti za chakula na lishe zenye lengo la kupunguza utapiamlo, kudumaa kwa ukuaji wa watoto na kuanzisha tafiti za chakula na lishe zinazolenga kuwawezesha watoto kupata lishe bora kuwa na maendeleo ya mtaji wa watu katika uchumi wa ushindani.
''Serikali ipo tayari kuwawezesha wawekezaji kuanzia viwanda vidogo hadi vikubwa, lakini pia kwa sasa hivi wapo wazalishaji wa mtu mmoja mmoja hususani wanaotengeneza unga na chumvi majumbani, wote hao ni watu muhimu kwetu,"amesema Majaliwa.

Aidha, aliwataka wadau wa lishe nchini kuanzia ngazi ya mtaa, halmashauri na Taifa kusimamia na kutekeleza kwavitendo kaulimbiu ya serikali ili kuleta mafanikio ,

"Napenda niwaambie wadau wetu wa lishe kuwa tutekeleze kwa vitendo kaulimbiu yetu ili tupate matokeo chanya kwenye taifa letu, tuweke virutubisho kwenye usindikaji wa vyakula,"amesema.

Amesema, ripoti ya Chakula na Lishe ya mwaka 2018 nchini Tanzania inaonyesha kuwa licha ya uvunaji wa mazao kuwa mkubwa, lakini utapiamlo na kudumaa kwa kasi ya ukuaji katika mikoa na miji ya uzalishaji wa kilimo kwa asilimia kwenye mabano ni Njombe (53.6) Rukwa (47.9) Iringa (47.7) Songea (43.3) ) Kigoma (42.3) Ruvuma(41.0) na Tanga (31.8).

“Tanzania tuna watafiti, lakini hakuna utekelezaji kwa walichokitafiti, hivyo ni muhimu kwa taasisi za juu za Tanzania zinazofanya utafiti kuanzisha utafiti wa masuala ya chakula na lishe wenye lengo la kutoa matokeo chanya na nitoe wito kwa serikali, sekta binafsi, wizara. na mashirika ya kimataifa kushirikiana katika suala hili, tutafanikiwa.

“Ndugu zangu watanzania wenzangu madhara yanayotokana na udumavu hayana tiba ni ya kuyadumu kwa kipindi chote cha uhai wa mtoto aliyeathirika serikali ya wamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Rais wetu mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini,”amesisitiza Waziri Majaliwa.
Waziri Majaliwa ametoa wito kwa watanzania wote kuwa wafuate maelekezo ya wataalamu wa afya na kwa pamoja washirikiane kupambana na changamoto ya udumavu, lengo likiwa ni kuifanya nchi kuwa ya uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda maendeleo ambayo hayawezi kupatikana iwapo hawatajenga kizazi chenye nguvu,afya njema na uwezo wa kufikiri.

Amesema, serikali imeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji wa usindikaji wa bidhaa lishe hapa nchini,

"Rasilimali watu ndio msingi mzuri wakutokomeza umaskini nchini kwetu lakini pia lishe bora ndio msingi wa afya za watu na husaidia kuipunguzia serikali mzigo wa gharama za kimatibabu kwa wananchi wake,"amesisitiza Majaliwa.

Kwaupande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, alisema baadhi ya mikoa nchini mpaka hivi sasa inaendelea kuongoza kwenye udumavu kutokana na lishe duni kuwa ni mkoa wa Njombe 53.6%, Rukwa 47.9%, Iringa 47.1%, Songwe 43.3% kigoma 42.3% na Ruvuma 41.1% .

Amesema, elimu juu ya lishe inapaswa kutolewa kwa wananchi ili kuweza kutumia vyakula wanavyolima wenyewe kwa lengo la kuondokana na utapiamlo ikiwemo udumavu.

Aidha ametoa maagizo kwa Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwasimamia kwa dhati makatibu wote wa Mikoa na Halmashauri za Wilaya ili kutekeleza mikataba ya lishe iliyokubaliwa Agosti 10,000 kwa ajili ya kulisha watoto na kushirikiana na wadau wote wa chakula na lishe. sekta kwa kuongeza uzalishaji wa chakula.

Waziri Mhagama amesema, takwimu za utapiamlo zinatishia na kuagiza sekta zote za chakula zinazohusika na uzalishaji wa chakula na lishe kuwajibika katika suala hilo.
Katika kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Ummy Mwalimu alikubali kufuatilia fedha zinazotolewa kwa ajili ya chakula na lishe kwa watoto zinazotolewa na Halmashauri za Wilaya kwa mujibu wa makubaliano na kutoa onyo kali kwa watendaji watakaoelekeza fedha hizo kinyume.

Pia aliiomba Serikali kuiagiza Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoa kibali cha kuajiri Maafisa Lishe 90 ili kufidia upungufu wa watumishi 94 ambao wakati mwingine unafanya utekelezaji wa programu za lishe kudorora.

Post a Comment

0 Comments