Watakiwa kuongeza kasi ukusanyaji kodi ya pango la ardhi

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kuongeza kasi ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dk. Angeline Mabula akikagua majalada ya ardhi katika ofisi ya ardhi Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga hivi karibuni. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Clemence Nkusa na kulia ni Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa hiyo, Yusufu Luhumba.

Hatua hiyo inafuatia Dkt.Mabula kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya ardhi ambapo Manispaa hiyo ya Kahama hadi kufikia Novemba mwaka huu imekusanya milioni 460,328,934 kati ya bilioni 3.5 ilizopangiwa kukusanya katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Kwa mujibu wa Afisa Ardhi Mteule Manispaa ya Kahama, Bw. Yusufu Luhumba katika kipindi cha mwaka uliopita wa 2020/2021 Halmashauri ya Manispaa hiyo ya Kahama ilipangiwa kukusanya bilioni 2.5 lakini ilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.330 sawa na asilimia 53.25.

Aidha, Manispaa hiyo inawadai wamiliki wa ardhi kiasi cha bilioni 1.6 ambapo Naibu Waziri wa Ardhi alielekeza manispaa hiyo kuhakikisha anawachukulia hatua wale wote walioshindwa kulipa madeni ya kodi ya pango la ardhi kwa wakati kwa kuwa wamevunja masharti ya umiliki.

Hata hivyo, Dkt.Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kabla ya kuwafikisha wadaiwa katika mabaraza ya ardhi kuzungumza nao ili kuangalia namna bora ya kulipa madeni hayo na kuongeza kuwa, iwapo wapo wadaiwa wanaoweza kulipa kwa awamu basi mazungumzo yafanyike lakini kwa kuzingatia fedha kulipwa kwa kuzingatia kipindi cha mwaka wa fedha husika.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Clemence Nkusa wakati wa ziara yake katika manispaa hiyo hivi karibuni.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya Kahama akiwa katika ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Shinyanga hivi karibuni, Dkt.Mabula alisema, wale wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi walioshindwa kulipa madeni yao wanatakiwa kufikishwa katika mabaraza ya ardhi ili washitakiwe kwa kushindwa kulipa.

”Maelekezo yangu wale wote walioshindwa kulipa madeni yao basi sheria ichukue mkondo wake ikiwemo kuwafikisha katika Mabaraza ya Ardhi ambako huko maamuzi ni kulipa ama mali za wahusika kupigwa mnada kufidia deni,”alisema Dkt.Mabula.

Aidha, Dkt.Mabula aliitaka halmashauri ya Manispaa ya Kahama kuhakikisha inatumia vyombo vya habari pamoja na ujumbe wa simu kuwakumbusha wamiliki wa ardhi katika Manispaa hiyo kulipa kodi ya pango la ardhi ili waweze kulipa kwa wakati na kuiwezesha serikali kupata mapato.

Awali, Afisa Ardhi Mteule Yusufu Luhumba alisema, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imeendelea na utaratibu wa kuwafuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi na jumla ya thamini 37 za wadaiwa kati ya 103 zimekwishakabidhiwa kwa dalali wa mahakama kwa utekelezaji.

”Wakati thamini 54 zimekwisha andaliwa na kukamilika, kwa sasa zinasubiri kusainiwa na mthamini Mkuu wa serikali kisha kupelekwa kwa dalali wa mahakama kwa utekelezaji wa uuzaji,”alisema Luhumba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news