Wavalia madera usiku na kuwabaka wanawake mjini Sumbawanga

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wanawake wa Kata ya Mafulala Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikia baadhi ya wanaume katika kata hiyo kuvaa madera ili wasijulikane jinsia zao huku wakitekeleza vitendo vya ubakaji majira ya usiku.

Hayo wameyasema katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na diwani wa kata hiyo, Lameck Mpondela ili kusikiliza kero zao.
Dera ambalo ni vazi linalopendelewa zaidi kuvaliwa na wanawake wa ukanda wa Pwani, kwa sasa baadhi ya wanaume wanatuhumiwa kulivalia ili kutenda maovu mjini Sumbawanga.

Wananchi wa kata hiyo wamesema kuwa, lengo la wanaume hao kuvaa madera ni kufanana na wanawake ili wasiweze kugundulika pindi wanapowabaka wanawake.

Miongoni mwa wanawake hao ni Elizabeth Kanyengele mkazi wa kata hiyo ambaye amesema kuwa, watu hao wamekuwa pia wakivamia nyumba za wajane nyakati za usiku na kufanya vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikihatarisha usalama na maisha yao.

"Tunaomba muheshimiwa diwani utusaidie, wanatuingilia sisi wajane, wakiwa wamevaa madera na kutufanyia vitendo vya kinyama, tunaomba sana tusaidiwe maana maisha yetu yapo mashakani kutokana na kuibuka kwa matukio hayo,"amedai.

Daniel Mwanakatwe ambaye ni mkazi wa kata hiyo amesema kuwa , watu hao kwa kuwa wanakuwa wamevaa madera, mwanamke anapomuona kwa mbali anajua naye pia ni mwanamke hivyo anaondoa hofu, na anapopita kichochoroni nyakati za usiku anabakwa na mtu huyo.

"Tunaomba kama inawezekana tuanzishe hata kikundi cha ulinzi, wachaguliwe vijana 20, tuwe tunalinda maana sasa wake zetu wako hatarini na watu hawa wanaweza kutusababishia hata magonjwa katika ndoa zetu,"amesema Diwani wa kata hiyo.

Mpondela amesema kuwa, amepokea malalamiko yote na anaahidi kuyafanyia kazi na atawasiliana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia malalamiko hayo, Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, William Mwampaghale alikiri kutokea tukio moja la kubakwa mama mmoja mjane ambapo mtuhumiwa aliingia ndani ya nyumba yake usiku, akampiga na kumbaka na Jeshi la Polisi linamsaka kwa kuwa anafahamika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news