Ziara ya Waziri Mkenda yaonyesha mwanga mpya kwa wakulima wa michikichi nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

ZIARA ya Waziri wa Kilimo,Prof. Adolf Mkenda nchini Uganda akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Mhe. Thobias Andengenye, Mkurugenzi wa Maendeleo Mazao wa Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu na wataalam wengine wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma imeonyesha mwanga mpya kwa wakulima wa michikichi nchini.
Mwanga huo umeonekana, baada ya siku ya pili ya ziara hiyo, Waziri kusisitiza kuwa, wizara yake imejipanga katika kuhakikisha inampatia mwekezaji eneo la kuwekeza kwenye zao la michikichi.

Sambamba na kutoa elimu kwa wakulima na kuwasaidia kifedha ili kuhakikisha nchi inapunguza ama kumaliza kabisa changamoto ya kuagiza mafuta ya mawese kutoka nje ya nchi. TAZAMA VIDO CHINI
Prof.Adolf Mkenda ameyabainisha hayo Novemba 25, 2021 wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mafuta cha Kampuni ya Oil Palm Uganda Limited kilichopo katika kisiwa cha Kalangala nchini Uganda wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne nchini humo.

Amesema kuwa, Serikali itaimarisha mfumo wa kilimo cha michikichi kwa kuhakikisha kuwa inatoa elimu ya kutosha kwa wakulima kwa utaratibu ambao utahusisha mashamba makubwa na mashamba ya wakulima wadogo ili kuwa na kilimo chenye tija kinachowahakikishia soko la uhakika katika viwanda.

"Katika siku ya pili ya kutembelea mashamba na viwanda vya michikichi, kiwanda hiki hapa kimewekwa karibu na mashamba ya watu binafsi (out growers). Ambao wenyewe wanavuna na kuleta kiwandani, kwa ajili ya kutengeneza mafuta.

"Ni mfumo ambao unamuweka mwekezaji anakuwa na shamba lake kubwa ili aweze kuzalisha vya kutosha kuhakikisha kwamba, kweli anaweza kuweka kiwanda.Lakini anatoa fursa kwa wakulima wenyewe kulima michikichi na kuhakikisha kwamba wanaweza kuuza matunda yao hapa kwa ajili ya kukamua mafuta.

"Kitu ambacho tumekielewa hapa ni kwamba katika mfumo kama huu, ni muhimu sana wakulima waweze kupata mafunzo ya kutosha,lini? Wakati wa kuvuna ili kufahamu mavuno yawe na ubora gani, ili kuhakikisha kweli kila tunda linakuwa na mafuta ya kutosha. Endapo kuna wakulima ambao watalima bila kupata mafuta ya kutosha, watalima halafu bei itashuka chini, kwa hiyo watakuwa wanawaumiza wengine ambao wanalima vizuri.

"Kwa hiyo tutakapoingia katika mfumo huu, tutaongeza bidii kubwa kuhakikisha wakulima wanapata mafunzo ya kutosha, kwa sababu hatutapenda kuona kuna mashamba ya wawekezaji halafu wakulima waachwe solemba, halafu wafanywe kama vibarua wameajiriwa, tunataka mwekezaji akiwepo wale wakulima waliopo pale, waweze kuotesha nao michikichi yao kwa utaratibu ambao wizara itakuwa inawasaidia, halafu vilevile tuwape mafunzo ili waweze kuuza matunda yao katika kiwanda kama hiki.

“Mtazamo wetu sasa hivi tutakaporudi nyumbani tumewaomba mwezi wa 12 waende mkoa wa Kigoma na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ameanza kuona sehemu ambayo itatusaidia kuwapa eneo kwenda kuwaandaa wakulima wa kule kwa ajili ya kujipanga kuandaa mashamba. TAZAMA VIDEO CHINI
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye amesema kuwa, wamekuwa wakiwaambia wananchi wao kuwa, moja kati ya mazao ambayo hayatawasumbua kupata soko ni pamoja na mafuta ya mawese.

"Lakini pia ni ni zao ambalo halina usumbufu katika kuliendesha,ukiachia uvumilivu wa ile miaka mitatu ya mwanzo, baada ya hapo si kama mazao mengine ambayo yanakulazimisha kukaa shambani wakati wote,ninaamini fursa hii wananchi wa Kigoma walikuwa wanaisubiria kwa muda mrefu ya kuleta mapinduzi ya teknolojia mpya kutoka kwa watu ambao wamefanikiwa,"amesema RC Andengenye.

Mhe.Andengenye amesema kuwa, Kigoma ni mkoa ambao una eneo kubwa la kilimo na hali ya hewa rafiki kwa kilimo cha michikichi, hivyo mkoa huo unaweza ukawa ndio wazalishaji wakubwa Afrika nzima endapo wakulima wakiwezeshwa na wawekezaji wakijitokeza kuwekeza kwa wingi.

Post a Comment

0 Comments