Dkt.Grace Magembe asisitiza ubora, kuzingatia muda ujenzi wa EMD na ICU

NA ASILA TWAHA, OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya) Dkt. Grace Magembe amewataka wataalam wa Afya wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuepuka migogoro isiyoleta manufaa katika kusimamia ujenzi wa miradi ya ujenzi wa EMD na ICU.
Wito huo ameutoa Desemba 3, 2021 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha kuwajengea uwezo Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, Waganga Wafawidhi na Wahandasi katika kusimamia miradi ya ujenzi wa majengo ya dharura (EMD) na ICU.

Dkt.Grace amesema, siku walizokuwepo katika kikao hicho wanaporudi kwenye vituo vyao vya kazi waende wakashirikiane kwa kusimamia na kutekeleza miradi ya ujenzi wa EMD na ICU kwa ubora na wakati lengo likiwa ni wananchi waweze kupata huduma kwa haraka.

Pia amesema, OR-TAMISEMI imetengewa shilingi bilioni 493.9 sawa na asilimia 38 na fedha zote hizo ni kwa sababu ya sekta zilizopata athari za kiuchumi kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19.

Aidha, amesema fedha zilizotolewa shilingi bilioni 236 kwa upande wa afya ni kutekeleza miradi inayolenga kujikinga ugonjwa wa UVIKO-19 ikiwemo miradi ya ujenzi wa majengo ya dharura na ICU.
Akiendelea kufafanua Dkt. Grace amesema kuwa, fedha hizo zimeelekezwa kutekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na athari za UVIKO-19 ikiwemo ujenzi wa ICU 26, EMD 80, ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa (ambulances) 195, ujenzi wa mitambo mikubwa 6 ya kuzalisha oksijeni ambapo itakuwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 200 kwa saa 24 na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya kuimarisha huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Natoa wito twendeni tukasimamie, wananchi wanataka huduma sio mivutano asiye taka kufuata utaratibu kwa wakati hatua zitachukuliwa na ujenzi wa ICU na EMD unatakiwa usimamiwe kwa umakini ukikosea ujenzi maana yake hata kutoa huduma utakosea,” amesisitiza Dkt. Grace.

Mganga Mkuu wa Mkoa Mara, Dkt. Juma Mfanga ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha za miradi ya ujenzi wa EMD na ICU na kuihakikishia wanaenda kushirikiana kwa ukaribu na watendaji wote wakiwemo na wahandisi ili kazi hiyo ifanyike kwa weledi, ubora na kukamilika kwa wakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news