Hoja ya Rais Samia kuhusu makundi ndani ya Serikali yamuibua Dkt.Kigwangalla, asema baada ya Bunge kusema Januari, mwakani naye atasema ukweli

NA GODFREY NNKO

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema, anafarijika kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameanza kuujua ukweli wa mambo.
Mheshimiwa Dkt.Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nzega mkoani Tabora ameandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa;

"Nashukuru mama sasa ameanza kuupata ukweli wa mambo, tutafurahishwa muda si mrefu. Kuna watu walituchongea, wakatuchafua, wakatusimanga na kutusingizia mambo mengi ya uongo tu kwa kuwa walikuwa na access, sasa ya kwao yenye ‘ushahidi’ wa wazi yanajulikana! Mungu mkubwa sana,", ameandika Mheshimiwa Dkt.Kigwangalla.
Ujumbe huo ameutoa baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kubainisha kuwa, kuna makundi ya watu ndani ya Serikali wamekuwa wakifanya mambo ya ovyo jambo ambalo linarudisha nyuma utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Samia amesema hayo Desemba 4, 2021 wakati akizungumza alipohudhuria uzinduzi wa maboresho ya gati namba 1 hadi namba 7 ya Bandari Kuu ya Dar es Salaam.

“Kuna makundi wanajua wanayoyafanya ndani ya serikali…ni makundi hayo hayo yanageuka kusema serikali awamu ya sita ufisadi umerudi, mambo yako hovyo…kumbe wao ndio wako ovyo.

“Na mambo yale hayakufanyika ndani ya Awamu ya Sita, yalifanyika huko nyuma, gari bovu linaangushiwa Awamu ya Sita… sitakubalii… sitakubali," amesema Rais Samia.

Aidha, baada ya ujumbe huo aliouandika Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla na kuusindikiza na video vifupi ya Mheshimiwa Rais, wafuasi wa Mbunge huyo walianza kutiririka mambo mazito.

Miongoni mwao ni Wakili Fatma Karume ambaye amemtaka kueleza kuhusu tuhuma zinazomuhusu kutokana na ripoti ya CAG.

"Hamisi, naomba utueleze Mama kugundua haya kuhusu wengine, yanafuta Ripoti ya CAG dhidi yako? Maana hii “defence” sijaielewa hata kidogo,"Wakili Fatma Karume amemuhoji Mheshimiwa Dkt.Kigwangalla.
Baada ya swali hilo, Mheshimiwa Dkt.Kigwangalla amejibu kuwa "Fatma, ondoa shaka na mimi. Siyo mwizi wala mpiga deal. Ni kwa vile sijajitetea, na ni kwa sababu ninajiamini.

"Niliamua kuheshimu mamlaka ya CAG kutoa taarifa zake wakati ule. Bunge litasema January kama kuna kitu ama la, na mimi nitasema January. Ikibidi nitasema ziada kidogo,"ameeleza Dkt.Kigwangalla.

Post a Comment

0 Comments