Hope for Girls and Women in Tanzania( HGWT) kutoka Mara latwaa tuzo kwa kuwa kinara mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji pamoja aina mbalimbali za ukatili lenye makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara limeshinda Tuzo ya Ruzuku.

Ni kutokana na kuwa kinara wa kupinga ukatili wa kijinsia na hivyo jitihada za dhirika hilo kutambuliwa na kuthaminika kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly (kulia) akiwa na viongozi wa mashirika yaliyoshinda Tuzo ya Ruzuku na kupewa tuzo katika tamasha lililofanyika ukumbi wa Serena Hotel jijini Dar es Salaam,Desemba 8, 2021.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly.

Tuzo hizo zilitolewa Desemba 8, 2021 katika ukumbi wa Serena Hotel jijini Dar es Salaam ambapo mashirika sita yalifanikiwa kushinda tuzo hiyo katika Siku 16 za uanaharakati wa kupinga ukatili wa Kijinsia "A joint champions Award and Concert on 16 days of Activism against Gender Based -Violance with over 30 artists sports Champs and activities" katika tamasha lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Ambapo mashirika mengine yaliyoshinda tuzo hiyo ni pamoja na KIVULINI la jijini Mwanza, Agape Organization la Shinyanga, Tanzania's Media Women's Association (TAMWA)-Zanzibar, Shika Ndoto la Dar es Salaam pamoja na DMI Spring of Hope Dar es Salaam.

Tuzo hizo ziliandaliwa na taasisi za Umoja wa Mataifa ambazo ni UN Women, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Umoja wa Ulaya pamoja na Balozi mbalimbali hapa Tanzania ambapo zinalenga kutambua na kuthamini juhudi za mashirika yanayopambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo yao na taifa kwa ujumla ambapo pia yatapokea fedha zilizokusanywa katika warsha hiyo ili ziwezeshe juhudi za mashirika hayo kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Rhobi Samwelly ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania ambaye alishawahi kutunukiwa tuzo ya heshima ya malkia wa nguvu kutokana na mchango wake kutambuliwa katika kutetea haki za binadamu akizungumza na DIRAMAKINI BLOG amesema kuwa, anashukuru kupokea tuzo hiyo na kwamba ni jambo la heshima na faraja Kutokana na jitihada za Shirika la HGWT kutambuliwa na kuthaminiwa kitaifa na kimataifa na hivyo akaeleza kuwa atahakikisha anaendeleza juhudi hizo katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali.

Amesema, tuzo hiyo imempa hamasa kubwa na kwamba atazidi kuhakikisha kwamba anasimama kidete kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji, vipigo kwa wanawake, pamoja na mila kandamizi ambazo bado ni kikwazo katika jamii huku akiomba wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuwafichua wahusika ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Aidha, Rhobi aliongeza kuwa, kila mmoja ana wajibu wa kushiriki vyema katika mapambano ya Ukatili wa Kijinsia akasisitiza kuwa, Taifa linahitaji wasomi wa kuliletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hivyo wazazi na walezi wote wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuwasomesha watoto wa kike kwani wana mchango mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na siyo kuwaoza kabla ya kutimiza ndoto zao.

"Namshukuru Mungu kwa neema hii ambayo Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limeweza kuwa miongoni mwa mashirika sita yaliyoshinda tuzo hii. Kwangu ni heshima kubwa na pia inanipa mimi binafsi na wenzangu kutoka mashirika mengine chachu kubwa na ari katika kuendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia. Naahidi kwenda kufanya kazi kikamilifu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Dawati la Jinsia, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii Polisi na Asasi zote za Kiraia kwa kushirikiana na Serikali ili kutokomeza ukatili," amesema Rhobi.

Juma Mathias ni mkazi wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara akizungumzia hatua ya shirika hilo kushinda tuzo hiyo amesema, analipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kutwaa tuzo hiyo, kwani limekuwa msaada mkubwa katika kupigania haki za binadamu kwa kiwango kikubwa sana hasa kuwapa hifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu kinachomilikiwa na shirika hilo.
Neema Marwa mkazi wa Mugumu akiongea na DIRAMAKINI BLOG amesema,shirika hilo pia limeongeza uelewa kwa wanannchi kwani limekuwa likitoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya mikusanyiko, kutumia ngoma za asili, michezo, na kufika katika shule mbalimbali kutoa elimu na hivyo hivi sasa wananchi wengi wameweza kuwa na ufahamu juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia.

"Mdogo wangu alikimbia ukeketaji miaka ya nyuma kidogo akaenda kupata hifadhi katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini kilichopo chini ya shirika hilo, alilipiwa ada akasoma chuo cha ushonaji kwa baadaye aliporudishwa nyumbani alikuwa amejua kushona vizuri kwa sasa ni fundi anahudumia familia yake na pia wazazi wetu anawasaidia hata Mimi wakati mwingine ananisaidia. 

"Kwa hiyo kumbe ukatili hauna faida kama asingekimbilia kituoni hapo asingekuwa tegemeo kama ilivyo sasa," amesema Neema Marwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news