Mheshimiwa Othman asisitiza umoja na mshikamano ili kufaidi matunda ya Uhuru

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema dhamira ya Uhuru ni kuwapatia wananchi haki, heshima, usawa, maendeleo na huduma bora za msingi ili kujitegemea kiuchumi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Desemba 6,2021 akiwa Mgeni Rasmi na Mshiriki Maalum wa Majukwaa mawili ya Kitaifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila.

Huko ameshiriki na kulifunga Kongamano la Kutimia Miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, na baadaye hafla ya Uzinduzi wa Jengo jipya la Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika ya Mashariki, kinachosimamiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili.

Amesema, dhamira hiyo ya dhati na matunda ya kujivunia yaliyopatikana ni kutokana na juhudi za makusudi za Waasisi wa Taifa hili, za kupigania heshima ya Mtanzania kupitia misingi ya utu na utawala unaozingatia haki na sheria.

Aidha, amesema kuwa ili Tanzania kufikia utekelezaji wa malengo ya ukombozi katika mafanikio bora ya maendeleo ya kiuchumi, kama ilivyo kwa mataifa mengine, inalazimika kuzingatia uwepo wa taasisi makini na imara, zilizojengwa kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na uadilifu.
Akiwa Kampasi ya Mloganzila, Mheshimiwa Othman ameshukuru juhudi za Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) iliyotoa Mkopo wa masharti nafuu kusaidia utekelezaji wa azma ya Afrika Mashariki kuwa na Taasisi ya Mabingwa wa Maradhi yasiyoambukiza, huku akiahidi mkono wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhakikisha Kituo hicho kinakidhi mahitaji na kutekeleza malengo yake.

Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam (UDSM) na Muhimbili ( MUHAS), Prof William Anangisye na Prof Andrea Pembe, wameeleza hatua kwa hatua ambazo Watanganyika wamepitia tangu wapate Uhuru wa Disemba 1961, katika sekta za elimu, afya, mahusiano ya kimataifa, usawa na jinsia, zikiashiria nia ya dhati ya kupigania maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba akitoa neno katika kongamano hilo amehimiza haja ya kuwa na umoja wenye dhamira ya kweli, ili kubaki na Tanzania ya kujivunia kwa kizazi kijacho.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Lazaro Ndalichako, ameziambia hadhara zote mbili, juhudi za Serikali ya Tanzania kuwafikishia wananchi huduma muhimu, zikiwemo hatua ya ujenzi wa madarasa 15,000 ya shule kwa wakati mmoja, ambayo haijawahi kutokea, katika kile alichotaja kuwa ni sehemu ya kufaidi matunda muhimu ya uhuru.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa mbele ya wasomi na wanataaluma zikiwemo Miaka 60 ya Uhuru katika Maendeleo ya Kiuchumi, Sekta ya Afya na Elimu, Tanzania katika Ushirikiano wa Kimataifa, Wanawake na Uongozi, Mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Afrika, na Miaka 60 ya Uhuru katika Amani, Ulinzi na Usalama.

Waliowasilisha mada hizo ni pamoja na Wasomi na Wanadiplomasia Wabobezi wakiwemo Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, Dkt. Godbertha Kokubanza Kinyondo, Balozi Brigedia Jenerali Fracis Benard Mndolwa, Prof Bernadeta Killian Mchapwaya, Balozi Dkt. Mohammed Omar Maundi, na Meja Jenerali Ibrahim Mhona, chini ya uongozaji na uamidi wa Profesa Rwekaza Mukandala na Dkt.Ayub Rioba.

Viongozi mbali mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Wasomi, Wanataaluma, Washirika wa Maendeleo, Vyama vya Siasa na Waandishi wa Habari walihudhuria hafla hizo wakiongozana pia na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Heri James, Naibu Waziri wa Afya Tanzania Bara, Bi Mwanaidi Ali Khamis, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dkt. Omar Dadi Shajak na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Muhimbili, Dkt.Harrison Mwakyembe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news