Muongozo wa uendelezaji maeneo ya malisho wazinduliwa

NA ROTARY HAULE

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, amezindua muongozo maalum wa Upatikanaji, Usimamizi na Uendelezaji wa maeneo ya malisho ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto za migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.
Ndaki, amezindua mpango huo mjini Kibaha mkoani Pwani kwa kuwashirikisha wakuu wa mikoa mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko,Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere,Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera,Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella pamoja na Charles Ibuge kutoka Ruvuma.

Mbali na viongozi hao, lakini wengine walioshiriki katika uzinduzi wa mpango huo ni pamoja Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, wakulima,wafugaji,taasisi za kiraia, wataalamu wa malisho ya mifugo pamoja na wadau wengine.

Awali akizungumza kabla ya kuzindua mpango huo, Waziri Ndaki,amesema kuwa uzinduzi wa mpango huo unatokana na chimbuko la ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)ambayo inataka mpaka kufikia mwaka 2025 Tanzania hiwe na eneo la malisho hekta milioni 6.

Amesema,ilani inaelekeza kuwa lazima kuyabaini,kuyatenga na kuyamilikisha kwa ajili ya malisho ya mifugo ili kuondoa changamoto na migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

"Suala la malisho ni changamoto kubwa kwa nchi yetu na hii ni sababu ya kuwa na mifugo mingi,watu wengi, shughuli za watu kuwa nyingi na ardhi ni ileile ya Mungu,"amesema Waziri Ndaki.
Ndaki ameongeza kuwa nchi inahitaji hekta za malisho milioni 103 lakini eneo lililokuwepo ni hekta milioni 90 kwahiyo ikifumbiwa macho Mambo yatakuwa hayaendi sawa kwakuwa mifugo yote iliyopo nchini ni milioni 67 huku Watanzania wakiwa zaidi ya milioni 60.

Amesema, kutokana na changamoto hiyo Serikali imeamua kuja na mpango na muongozo wa pamoja ambao unakwenda kumaliza changamoto za wafugaji na hata wakulima waliopo nchini.

Amesema, muongozo huo unafaida nyingi na kwamba mbali na kupunguza migogoro Kati ya wakulima na wafugaji pia itakuwa ni msingi na fursa ya wafugaji kuelewana namna ya kufuga kisasa na kwa tija.

Amesema,faida nyingine ni kusaidia uzalishaji mbegu za malisho,kueneza teknolojia ya malisho ya mifugo kwa wafugaji na hata kuhamasisha wakulima kulima malisho ya mifugo kwakuwa itakuwa njia ya kujipatia kipato.

Hata hivyo,Waziri Ndaki amewashauri wafugaji kuhakikisha wanapokwenda kutekeleza muongozo huo lazima wakubali kutunza vyanzo vya maji, wafugaji waanze kuvuna mifugo yao sambamba na kubadili fikra zao kuwa mifugo ni zao ambalo wataweza kuvuna na kuuza kama mazao mengine.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge amesema kuwa, Sekta ya Mifugo ni miongoni mwa kipaumbele kikubwa mkoani kwake huku akisema kwasasa tayari ameandaa mpango mkakati wa matumizi bora ya ardhi.

Kunenge amesema kuwa, muongozo unaozinduliwa mkoani kwake ni makubaliano ya Wakuu wa Mikoa wa maeneo ya mifugo na watahakikisha wanasimamia mpango huo ili huweze kufikia malengo.

Amesema,mpaka sasa Mkoa wa Pwani una jumla ya mifugo 671,149 lakini changamoto kubwa wale wafugaji wenye tabia ya kuhamahama huku akisema kuna haja ya kuzuia mifugo isiondoke ili iweze kuhesabiwa.

"Mifugo ikizuiwa itasaidia kujulikana mifugo hiyo inatoka wapi na pia hiyo itasaidia kufanya sensa ambayo itatoa takwimu za kuzifanya kazi lakini niombe tuangalie namna ya kuweka mazingira bora kwa wafugaji,"amesema Kunenge.

Kunenge ameongeza kuwa, wafugaji nao wanakabiliwa na kero ya hupatikanaji wa maji na wakirudishwa walipotoka hakuna pa kuwapeleka kwakuwa lazima watahangaika kutafuta maji kwa ajili ya mifugo yao.

"Wafugaji wapo tayari kuchimba visima vya maji lakini hawapewi maeneo ya kudumu ,mimi naomba tutafute Wafugaji wachache wa mfano tuwape maeneo wachimbe visima,tuwape mbegu za malisho na imani tukifanya hivyo itakuwa mfano kwa wafugaji wengine,"amesema Kunenge.

Aidha, Kunenge amesema Ng'ombe ni sehemu ya familia na hatuwezi kuwatenga lakini ili kukabiliane na hali hiyo ya kuhamahama Mkoa wa Pwani umejipanga kutumia ranchi ya mifugo ya Ruvu kwa kuweka ranchi ndogondogo ambapo mpaka sasa Kuna hekta 24000 zimemilikishwa wa wafugaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, amesema wengi wanaishi kwa kuhamahama lakini anaimani muongozo uliozinduliwa utasaidia kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji na pia kuondoa migogoro ya ardhi.

Mrindoko, ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hatua hiyo kubwa huku akitumia nafasi kukaribisha wawekezaji Mkoani kwake kwakuwa fursa ya uwekezaji wa viwanda vya nyama na ufugaji unaozingatia Sheria upo.

Hata hivyo,Mrindoko amesema maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho yataendelea kuheshimiwa na wapo tayari kutekeleza muongozo huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news