Serikali ya Awamu ya Sita yaonyesha nia kuvifungulia vyombo vyote vya habari vilivyofungiwa nchini Tanzania

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI imesema ipo mbioni kuvifungulia vyombo vya habari ambavyo bado vimefungiwa mara baada ya kumaliza mazungumzo yanayoendelea hivi sasa baina ya mamlaka na wahusika wa vyombo hivyo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju ameyasema hayo leo Desemba 7,2021 jijini Dar es Salaam wakati akizindua kikao kazi cha Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Ni kikao kinachofanya marejeo na kuchambua mapendekezo 252 ya haki za binadamu.

Mheshimiwa Mpanju amesema, lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anarejesha uhuru wa vyombo vya habari hapa nchini.

“Hili ni miongoni mwa mapendekezo mliyoyatoa, itakapofika Februari 14 (mwakani) tutasimama na kutaja mapendekezo ambayo Serikali itakuwa imeyakubali na mpaka sasa tayari mengi yameshafanyiwa kazi likiwemo la wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni.

“Uhuru wa vyombo vya habari ni jambo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan amelisimamia na anahitaji matokeo ya haraka. Tumeshakutana na wadau na jana tumekutana na mamlaka husika kupitia vifungu vyote kuhakikisha kwamba tunavifungulia vyombo vyote vya habari ambavyo vilifungiwa. Rais ameagiza lazima tumalize hili jambo,” amesema Mheshimiwa Mpanju.

Kwa upande wake,Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema Serikali ni muhimu ikubali mapendekezo ya kuondoa sheria ambazo zinaminya uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza nchini.

Pia amesema ni muhimu kukubaliwa mapendekezo ya kuzifanyia maboresho sheria zilizofungia magazeti, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 , Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na kuruhusu watoto wakipewa ujauzito kurejea shule nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news