Serikali yasitisha ujenzi holela katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara

NA HAPPINESS SHAYO-WMU

SERIKALI imeagiza wananchi wanaoendelea kujenga katika eneo linalozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kuacha mara moja ili kuruhusu wanyama kuendelea kuishi katika ikolojia hiyo bila kubugudhiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Wilaya ya Monduli, Mhe.Frank Mwaisumbe akivunja moja ya ukuta wa mwekezaji uliozuia wanyamapori kutoka nje ya eneo hilo, pembezoni mwa ziwa Manyara ilipo Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara katika Kijiji cha Migungani Wilaya ya Monduli.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo lililopo kwenye Kijiji cha Migungani B, Wilayani Monduli.

“Naelekeza uzio wote uliojengwa kuzunguka hili ziwa uvunjwe na mwekezaji yeyote tutakayemsikia anajenga uzio tutamchukulia hatua za kisheria” Mhe. Masanja amesisitiza.

Aidha , Mhe. Masanja amesema kumekuwa na migogoro mingi kati ya wananchi na hifadhi baada ya kuvamia maeneo ya wanyama inayopelekea wananchi hao kuvamiwa na wanyama wakali kama tembo na kuwaasa wananchi kuchagua maeneo mazuri ya kuishi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akivunja moja ya ukuta wa mwekezaji uliozuia wanyamapori kutoka nje ya eneo hilo, pembezoni mwa ziwa Manyara ilipo Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara katika Kijiji cha Migungani Wilaya ya Monduli.

“Ifike mahali wananchi wahamie kwenye maeneo ambayo watakaa bila kubughudhiwa,” Mhe. Masanja amesema.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo Mhe. Masanja amesema Serikali ina mpango wa kufanya tathmini ya mapito yote ya wanyama na wananchi wawe tayari kuyaachia ili kukuza utalii nchini Tanzania.

“Nakuelekeza Mkurugenzi fanyeni tathmini katika mapito yote ya wanyama ili kujua majengo na mali zote zilizopo ili tuwahamishe wananchi kwa kuwapa fidia ili wanyama hawa waweze kupita,” amesisitiza Mhe. Masanja.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akiwa ameongozana na wahifadhi na uongozi wa Wilaya ya Monduli kukagua kuta zilizojengwa na wawekezaji zilizozuia wanyamapori kutoka, alipofanya ziara ya kikazi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Kijiji cha Migungani Wilaya ya Monduli.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza katika kikao kati yake na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Wilaya ya Monduli, Mhe.Frank Mwaisumbe kuhusu eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kuvamiwa na wananchi na wawekezaji kwenye Kijiji cha Migungani Wilaya ya Monduli.

Pia ameelekeza Maafisa Uhifadhi kufanya operesheni ya kuwatoa wanyama walio kwenye vizuizi vya kuta pembezoni mwa ziwa Manyara.

“Naelekeza maeneo yote yenye hawa wanyama kuwepo na ulinzi na ninaelekeza kabla mwezi huu haujaisha watoeni hawa wanyama walio kwenye vizuizi ili wawe huru,” Mhe. Masanja amesema.

Mhe. Masanja amewataka wakazi wa kijiji hicho kushirikiana na serikali katika utunzani na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu athari za wananchi kuvamia eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kuvamiwa katika ziara yake ya kikazi kwenye Kijiji cha Migungani Wilaya ya Monduli.
Baadhi ya wanyamapori waliozagaa katika makazi ya watu baada ya kuzuiliwa na ukuta kutoka katika eneo hilo pembezoni mwa Ziwa Manyara Wilaya ya Monduli.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe.Frank Mwaisume amesema katika kikao cha awali kati yake na wahifadhi wamekubaliana wawe na kikao kila baada ya miezi mitatu ili kupitia maeneo yenye vibali vya ujenzi ili kutathmini kama eneo hilo ni ushoroba au la.

Amemtaka Diwani wa Kata ya Migungani Joseph Pareso kuwa na taarifa sahihi za watu wanaochukua ardhi katika eneo lake ili kuepusha migogoro inayojitokeza.

“Mheshimiwa Diwani lazima ajue nani amechukua ardhi, kiasi gani, maeneo gani na kwa sababu zipi,” Mhe. Frank amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news