Serikali,HGWT wakutanisha wadau kujadili mbinu za kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia Serengeti

NA FRESHA KINASA

SERIKALI ya Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kupambana na ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu wilayani humo katika Mkoa wa Mara wameendesha kongamano maalumu lililojumuisha wadau mbalimbali kujadiliana mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni.
Kongamano hilo limefanyika Desemba 13, 2021 likiendana sambamba na kuhitimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika ukumbi wa Kisare uliopo Mugumu wilayani humo chini ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt. Vincent Mashinji na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa wilaya hiyo pamoja na asasi za kiraia, wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wazee wa Kimila, ngariba wastaafu, viongozi wa dini, polisi, pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa, vitendo vya ukeketaji wilayani humo vimekuwa vikichangia kwa kiwango kikubwa matatizo mbalimbali yakiwemo magonjwa ya zinaa, ndoa za utotoni, utoro shuleni, matatizo kwa kina mama kujifungua na matatizo ya kisaikolojia na hivyo akasisitiza kuwa jamii iachane na vitendo hivyo kwani havina tija.
"Kwa gharama yoyote ile Wilaya ya Serengeti tumekubaliana kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya wilaya yetu. Hatutaki kuona vitendo hivi vikifanyika wadau wote kwa pamoja tuungane kukemea ukatili wa kijinsia hususani ukeketaji ambao bado upo kwa Wilaya ya Serengeti. Kila baada ya miezi mitatu kamati itakuwa ikikutana kufanya tathmini kujua vitendo vya ukatili ndani ya wilaya yetu iwapo vimepungua,"amesema Dkt. Mashinji.

Aidha, Dkt.Mashinji ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kusaidia kwa kiwango kikubwa katika mapambano ya ukatili wa kijinsia huku pia mahakama akisisitiza kusaidia kwa ufanisi kutafsiri sheria ili kuwatia hatiani wahusika wa vitendo hivyo.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Kamala amesema licha ya ukeketaji kuwepo kwa kiwango kikubwa wilayani humo, lakini jambo la kushangaza hakuna ngariba yeyote aliyefungwa ndani ya Gereza katika wilaya hiyo. Na hivyo ameomba wadau wa sheria ikiwemo ofisi ya mashitaka kusimama kidete kusimamia kesi za ukatili wa kijinsia, hatua ambayo itasaidia kuvimaliza katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly amesema, shirika hilo limeendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto, Ustawi wa Jamii na kwamba limeendelea kuwahudumia watoto wanaokimbilia katika Kituo cha Nyumba Salama kilichopo chini ya shirika hilo kwa kuwapa hifadhi, kuwaendeleza kielimu, kifani na kuwapa ushauri wa kisaikolojia.
 
Rhobi ameongeza kwamba, viongozi kuanzia ngazi za chini wana jukumu la kuendelea kuwajibika kutumia sheria kuwabana vikali wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji kwani vinarudisha nyuma juhudi za watoto wa kike kusoma ili wafikie ndoto zao na pia ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.

Amesema, shirika hilo kwa kutambua madhara ya Ukatili wa Kijinsia limeendelea na utoaji wa elimu kwa wananchi kwa njia ya mikutano ya hadhara shuleni na maeneo ya mikusanyiko pamoja na kuwaelimisha wazee wa kimila ambao wana nafasi kubwa ya kusaidia kutokomeza ukatili hususan ukeketaji.
Aidha, Rhobi ameongeza kuwa shirika hilo limefanikiwa kutumia teknolojia ya simu janja katika kupambana na ukatili wa Kijinsia ambapo katika Wilaya ya Butiama limetoa simu 94, Serengeti simu 107, na katika Wilaya ya Tarime simu 156 ambazo walipewa Mabalozi wa Shirika hilo na hutumika kuripoti matukio ya ukatili kupitaia APP maalumu iliyounganishwa na hivyo kuleta ufanisi katika mapambano ya vitendo hivyo.

Mchungaji wa Kanisa la Waandiventista Wasabato (SDA), Mugumu Richard Misogalya amesema, Biblia haikubaliani na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwamba kanisa hilo limekuwa likitoa elimu kwa waumini wake kupitia vipindi vya afya na kuweka msisitizo mkubwa kukemea Ukatili wa Kijinsia.

Naye Mchungaji Cleophas Nyamataga wa Kanisa la Mennonite Mugumu Serengeti amesema, suala la ukeketaji katika Wilaya ya Serengeti bado ni kubwa na ameomba viongozi wa kisiasa kulikemea vikali badala ya kulikumbatia kwa kuhofia kwamba wakilikemea watakosa kura nyakati za uchuguzi.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Serengeti, Veronica Lukanda amesema ili kutokomeza vitendo hivyo ni vyema wadau na wananchi wilayani humo wakishirikiana kutunga sheria ndogo kuanzia ngazi ya vijiji na Halmashauri na kwamba sheria hiyo itoe adhabu kali kwa watakaobainika kufanya vitendo vya ukeketaji na ukatili mwingine.

Rhoba Makonyo ni Mzee wa Kimila kutoka eneo la Kibanchebanche Wilayani humo, ambapo amesema kinachowafanya wazee wa Kimila kukumbatia mila ya ukeketaji ni kutokana na kuwaingizia kipato (fedha) na hivyo akashauri wazidi kuelimishwa na kutafutiwa njia nyingine ya kupata kipato.
Neema Paul Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti amesema, kwa mwaka 2020/2021 matukio 3,457 ya Ukatili wa Kijinsia yalilipotiwa yakiwemo ya ukeketaji, vipigo, ubakaji, ndoa za utotoni. akasema halmashauri imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na kutoa mafunzo kwa Kamati 109 zilizomo Wilayani humo za kutokomeza vitendo vya ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA).

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Serengeti, Wambura Sunday amesema kuwa kwa mwaka uliopita wanafunzi watoro kwa shule ya Sekondari walikuwa 701 na kwa shule ya Msingi walikuwa 2,866 jambo ambalo ni hatari kwa maendeo ya elimu.

Mathias Peter ni Makazi wa Mugumu amelipongeza Shirika la Hope kwa kushirikiana na serikali kuandaa Kongamano hilo kwani limetoa nafasi ya kujadiliana mambo mbalimbali yenye tija katika kutokomeza Ukatili.

Miongoni mwa mikakati ya kupambana na ukatili wa Kijinsia iliyojadiliwa na wadau Katika Kongamano hilo ni pamoja na elimu ya madhara ya Ukatili kutolewa kwa makundi yote, wadau wa ukatili wa Kijinsia wahudhurie mikutano ya viongozi wa kisiasa ili kuto elimu ya Ukatili, makanisa yasaidie kutoa elimu kwa waumini wao, wazee wa Kimila waelimishwe, vingozi wa chini washirikiane na vyombo vya usalama kuwafichua wahusika na kuripoti matukio ya Ukatili.
Mambo mengine ni pamoja na Nyumba Salama zinazohifadhi mabinti waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni zichukue mabinti wanaokimbia ukeketaji na uchunguzi ufanyike wakiwa nyumba salama, wanasiasa wasaidie kukemea Ukatili katika mikutano yao, zitungwe sheria ndogo kutoa adhabu kali kwa wanaofanya Ukatili wa Kijinsia, watuhumiwa wa ukatili wafikishwe mahakamani haraka wanapokamatwa, Wananchi wajitokeze mahakamani kutoa ushahidi ili kuwatia hatiani watuhumiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news