Ushirika ni fursa ya kuwainua kiuchumi wazalishaji wa maziwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KENNEDY Kisanga ambaye ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini amewashauri wazalishaji wa maziwa kuwa na ushirika imara wa maziwa ili kukuza na kupanua kilimo biashara.
Ameyasema hayo mjini hapa wakati alipokuwa akizungumza kuhusiana na mchango wa sekta ya ushirika katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Mchungaji Kisanga amesema tangu, Tanzania kupata Uhuru wake 1961, Sekta ya ushirika imekuwa na mchango mkubwa hususani katika kuwahamasisha watu wengi kujiunga na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na VIKOBA kwani katika miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa na vyama vya ushirika vichache kikiwemo Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU), Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (NCU), Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU).

“Ushirika ni biashara zinazojikita kwa watu, zinamilikiwa, zinadhibitiwa na zinaendeshwa na wanachama na kwa madhumuni ya kufikia mahitaji na malengo yao ya pamoja ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni,”amesema.

Mchungaji Kisanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa kituo cha kukusanya maziwa na kuyasindika cha Upendo Milk Centre kilichopo Sido Estate amesema kuwa, endapo wazalishaji wa maziwa wataweza kuunda umoja wao wa zao la maziwa, wataweza kukopesheka katika taasisi mbalimbali za kifedha.

“Katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ninawashauri sana wazalishaji wa maziwa tuweze kuunda ushirika wetu kama ambavyo ulivyo ushirika wa Kahawa, Pamba, Tumbaku, tutakapojiunga kwa pamoja na kuwa na ushirika wetu wa maziwa tunaweza kuwa na nguvu ya pamoja, lakini unapokuwa peke yako huwezi kuwa na maamuzi sahihi, lakini tunapokuwa wengi tunakuwa na sauti na hata tunaweza kufanya jambo na serikali ikatusaidia,”amesema Kisanga.

Amesema, licha ya Mkoa wa Kilimanjaro kuwa na vikundi vingi vya usindikaji wa maziwa, lakini hawajaweza kuwa na ushirika wao wa maziwa hivyo kuna haja ya kuona umuhimu wa kuunda ushirika imara wa maziwa, ili wakulima na wafugaji kuwa na sauti moja.

Amefafanua kuwa, ushirika wa maziwa, wakulima au wafugaji wanaweza kuokoa pesa kutokana na gharama za usafiririshaji wa maziwa kibinafsi, kupata mikopo ya kununua ng’ombe na pembejeo.

“Ili mfugaji aweze kupata faida hizi inamlazimu kujiunga pamoja na kuweka msingi thabiti wa kukuza ushirika hapa nchini hususani ushirika wa maziwa,”amesema Mchungaji huyo.

Pia Mchungaji Kisanga ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini, waliopo kwenye fani za mahesabu, kuanzisha vyama vya ushirika vya ukaguzi ili wawafanyie watu wengine ukaguzi katika vyama vyao, hali ambayo itawezesha kuondoa ubadhirifu ulipo katika vyama vya ushirika nchini.

Post a Comment

0 Comments