Wamisri nao wabisha hodi kuwekeza Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi apongeza hatua hiyo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uamuzi wa Kampuni ya Hoteli za Triumph kutoka nchini Misri wa kuja kuwekeza katika Sekta ya Utalii hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wawekezaji kutoka Makampuni ya Triumph Hotels Group kutoka nchini Misri, ukiongozwa na Meja Jenerali Ehab Shoman Mkurugenzi Mkuu wa Kanda wa hoteli hizo kulia kwa Rais akiwa na Ujumbe wake walipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar na kushoto kwa Rais ni Mkuu wa Kikosi cha KMKM Zanzibar Commodore Azana Hassan Msingiri.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kampuni hiyo uliongozwa na Meja Jenerali Ehab Shouman ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kanda wa Hoteli za Triumph kutoka nchini Misri.

Katika mazungumzo yake hayo, Rais Dkt Mwinyi umeuhakikishia uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inawawekea mazingira mazuri ili waweze kufikia azma yao waliyoikusudia katika kuekeza kwenye sekta ya utalii.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuueleza uongozi huo fursa zilizopo katika uwekezaji kwenye sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa visiwa vidogo vidogo ambapo Serikali imeamua kuviekeza kwenye sekta hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar mgeni wake Mkuu wa Ujumbe wa Wawekezaji kutoka nchini Misri wa Makampuni ya Triumph Hotels, Meja Jenerali  Ehab Shoman ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kanda wa Hoteli za Triumph, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Aidha, aliueleza uamuzi huo ni hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ndio Dira ya Uchumi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliupongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la KMKM na Jeshi la Misri na kueleza kwamba azma ya Misri kulisaidia Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) katika mafunzo na mambo mengineyo ya kuimarisha kikosi hicho yatasaidia kwa kiasi kikubwa.

Meja Jenerali Ehab Shouman ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kanda wa Hoteli za Triumph kutoka Misri kwa upande wake alimueleza Rais Dkt. Mwinyi azma ya kampuni hiyo ya kuwekeza hapa Zanzibar katika sekta ya utalii na kueleza jinsi walivyovutiwa na mazingira pamoja na mikakati ya uwekezaji iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Mwinyi.

Nae Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Komodoo Azana Hassan Msingiri alieleza mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya kikosi hicho na uongozi huo na kupongeza azma ya Misri ya kukisaidia kikosi hicho ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo kwa kikosi chake ili kuimarisha Sera ya Uchumi wa Buluu sambamba na kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji hao hapa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi (ZIPA), Sharif Ali Sharif alisema kuwa ugeni huo umekuja kwa azma ya kufanya mashirikiano na Serikali kupitia Kikosi cha (KMKM) na kuonesha nia ya kuekeza kwa kujenga hoteli yenye nyota tano, kuwekeza katika uvuvi pamoja na miundombinu ya ujenzi wa viwanja vya ndege.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news