Ajali ya gari la Magazeti yaua tisa, yajeruhi leo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WATU tisa wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali ya gari aina ya hiace ya kubeba magazeti iliyokuwa ikitoka jijini Dar es Salaam kuelekea jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa The Citizen, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema, ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Hiace lenye usajili namba T259 DWT mali ya Soma General Traders.

Waliofariki ni wanaume watano na wanawake wanne ambao wanafikisha idadi ya watu tisa.

Amesema, ajali hiyo imetokea leo Jumatatu Desemba 13, 2021 alfajiri katika Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Kamanda Bukumbi amesema, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambapo gari hilo lilimshinda dereva kwenye kona na kugonga mti uliokuwa pembezoni mwa barabara na kupinduka na kusababisha vifo vya watu tisa.

“Watu tisa wamepoteza maisha katika ajali hiyo ambapo wanawake ni wanne wanaume watano na majeruhi watatu wanaendelea kupewa matibabu katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa,"amesema Kamanda Bukumbi.

Kamanda huyo amesema, taratibu za awali zinafanyika kwanza ikiwemo utambuzi kabla ya kukabidhi miili hiyo kwa wahusika kwa ajili ya taratibu za maziko

Post a Comment

0 Comments