Wananchi wafunguka mbele ya Waziri wa Afya

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WANANCHI na wazazi wanaopata huduma kwenye kliniki ya watoto katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamemuomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongezewa wataalam wa huduma ya mishipa ya ubongo.
Wakizungumza mbele ya Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, leo Jumatano Desemba 29, 2021 mara baada kufanya ziara ya kutembelea kliniki ya watoto kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, na kuzungumza na wananchi na watoa huduma kisha kupokea maoni ya wazazi aliwaokuta wakipata huduma ndani ya kitengo hicho.

Wazazi hao wamemuomba yafanyike maboresho kwenye eneo la huduma za vyoo kwa ajili ya kuwasitiri watoto wadogo, kuwekewa feni ili kupunguza joto kwa watoto wadogo, kuongezewa mabenchi ya kukalia.

“Mheshimiwa tunaomba kuongezwa kwa wataalam wa huduma ya mishipa ya ubongo kwani uhitaji mkubwa,” amesema mmoja ya wananchi hao.

Kitengo hicho cha Mishipa ya fahamu pamoja na Ubongo, takwimu zinaonesha kinahudumia hadi watoto 80 kwa siku, Idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na Idadi ya Mabingwa waliopo kwa sasa.

Akijibu maswali ya wananchi na wazazi hao Dkt. Gwajima amesema ameyapokea maoni na mapendekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi.

“Ndugu zangu nimewasikia, uzuri hapa tupo na Mkurugezi anawasikia pia, lakini kama haitoshi, naomba niwape namba yangu ya kunitumia ujumbe mfupi, hii sio kwa ajili ya kupiga, niandikie ujumbe, tushauri nini tuweze kuboresha, kwa kutumia wataalam wetu tutachukua maoni yenu na tutayafanyia kazi,” amesema Dkt. Gwajima.

Post a Comment

0 Comments