Wawekezaji wenye viwanda nchini waalikwa kuwekeza jijini Dodoma

NA DENNIS GONDWE-DAR

WAWEKEZAJI wenye viwanda nchini wamealikwa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuchangia katika ukuzaji wa uchumi na ujenzi wa makao makuu ya nchi.
Afisa Mipango Miji wa Jiji la Dodoma, Aisha Masanja akielezea fursa za uwekezaji zilizopo katika Jiji la Dodoma kwenye Mkutano wa mwaka wa Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI) uliofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam. Katikati ni kiongozi wa timu ya kimkakati ya Uwekezaji na Masoko ya Jiji la Dodoma, Leonard Machunde na kulia ni Mchumi Mwandamizi katika Jiji la Dodoma, Abeid Msangi wakifuatilia kwa umakini mkubwa hali ya mambo katika wasilisho hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mipango Miji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alipokuwa akiwasilisha fursa za uwekezaji zilizopo katika Jiji hilo kwenye Mkutano wa Mwaka wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) uliofanyika katika hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.

Masanja alisema kuwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaunga mkono juhudi za serikali za ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini. 

“Katika kuunga mkono juhudi hizo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliandaa Mpango Kabambe wa miaka 20. Mpango huo umeainisha matumizi mbalimbali ya ardhi. Halmashauri imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Leo tunaleta kwenu fursa ya viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika eneo la viwanda Nala. Eneo la Nala lipo jirana na barabara kuu ya Singida, umbali wa kilometa 20 kutoka katikati ya mji,”alisema Masanja.

Akiongelea umuhimu wa eneo la viwanda Nala, alilitaja kuwa eneo hilo ni la kimkakati likiwa na miundombinu muhimu ya umeme wa msongo mkubwa, barabara na maji ya kutosha. 

“Eneo lina viwanja kwa ajili ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo. Eneo lina viwanja kwa ajili ya viwanda vya kufua umeme wa upepo, viwanda vya matengenezo ya magari, viwanda vya dawa, viwanda vya nguo na viwanda vya vyakula. Vingine ni viwanja kwa ajili ya viwanda vya chuma, viwanda vya mbolea na viwanja kwa ajili ya biashara,”alisema Masanja.

Kwa upande wa kiongozi wa timu ya kimkakati ya Uwekezaji na Masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leonard Machunde alisema kuwa eneo la viwanda Nala ni eneo la serikali chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. 

“Uzuri wa eneo hili, muwekezaji hatakiwi kupitia kwa dalali bali anakuja moja kwa moja ofisi ya Halmashauri ya Jiji kwa ajili ya kupata kiwanja. Hivyo, atapata kiwanja kwa gharama halisi. Gharama ya kiwanja ni shilingi 5,000 kwa mita mraba,” alisema Machunde.

Mchumi mwandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma aliwataarifu wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa CTI kuwa Nala ni eneo la kimkakati na sahihi kuwekezaji wa ujenzi wa viwanda. 

“Ni vizuri kuchangamkia fursa hii kuwekeza katika ujenzi wa viwanda katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi. Kadri unavyokuja mapema ndivyo unavyonufaika mapema. Makao makuu ya nchi lazima yatunufaishe wote,”alisema Mchumi Msangi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news