Waziri Mchengerwa akemea huduma mbaya zinazotolewa Hospitali ya Mkoa wa Kagera

NA JAMES K.MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amekemea huduma mbaya zinazotolewa kwa wananchi katika hospitali ya Mkoa wa Kagera.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisisitiza uwajibikaji kwa Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.

Akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, Mhe. Mchengerwa amesema, amekuwa akipokea malalamiko mengi ya wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo kuhusu huduma mbaya zinazotolewa hospitalini hapo.

Kufuatia malalamiko hayo, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki kukutana na watumishi wa hospitali hiyo kwa lengo la kuwahimiza waboreshe utendaji kazi wao.
Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Umma wa Umma wa Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.

“Nimepokea malalamiko mengi kupitia ujumbe mfupi na kupigiwa simu, watendaji wetu hawana lugha nzuri na utendaji kazi wao hauridhishi na kuna baadhi wanaomba rushwa kwa wananchi ili wawapatie huduma, hivyo tubadilike, turudi katika maadili ya taaluma ya kitabibu na misingi ya utoaji wa huduma bora.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kuboresha utendaji kazi katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.

Ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili katika hospitali hiyo, Mhe. Mchengerwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kagera kuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa lengo la kubaini changamoto wanazokutana nazo wananchi hao na kuchukua hatua stahiki.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, kutokana na huduma mbaya zinazotolewa na hospitali hiyo, inawalazimu baadhi ya wananchi kusafiri kwenda mkoa mwingine ili kupata huduma, jambo ambalo halileti taswira nzuri kwa umma na linawaondolea imani wananchi kwa serikali yao.
Mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Bw. Ezekia Nsinkala akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kufanya ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa katika Hopitali ya Mkoa wa Kagera, wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera.

Amesema,pamoja na kukemea kitendo hicho, atawasilisha malalamiko hayo kwenye mamlaka husika zinazosimamia taaluma za kitabibu ili nazo ziweze kufanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia taratibu zao za kitaaluma.

Mhe. Mchengerwa amehimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za kiafya zitakazoimarisha afya zao ili waweze kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa.

Post a Comment

0 Comments