Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman atoa rai kwa maafisa wa EWURA wanaoendelea na mafunzo

NA MWANDISHI MAALUM

MHESHIMIWA Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania amefungua mafunzo ya Kanuni na Mbinu za Usuluhishi wa Migogoro kwa maafisa kumi na tano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Washiriki wa mafunzo ya Kanuni na Mbinu za Usuluhishi wa Migogoro kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) wakiwa wanafuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo kutoka kwa Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani).

Mafunzo haya ya siku tano yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto yanafanyika kuanzia tarehe 17 Januari mpaka 21 Januari 2022 chuoni hapo.

Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Othman aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa mafunzo hayo ni fursa kwao kwani watabadilishana uzoefu kwa kuwa mafunzo hayo yamejumuisha washiriki enye taaluma mbalimbali na sio wanasheria peke yake. Aliendelea kwa kusema kwamba kwa hapa nchini usuluhishi katika migogoro mingi haifanywi na wanasheria bali na wanataaluma wengine.
Mhe. Mohamed Chande Othman Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania akifungua mafunzo ya Kanuni na Mbinu za Usuluhishi wa Migogoro kwa maafisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) hawapo pichani.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul. Kihwelo ameeleza lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo maafisa hao wa namna ya kusuluhisha migogoro mbalimbali kati ya watoa huduma na wateja. Mkuu wa Chuo aliongeza kwamba mafunzo haya yatasaidia kuongeza ufanisi katika eneo hilo la usuluhishi wa migogoro.

“Tunaamini mafunzo yatasaidia sana kuwajengea uwezo na kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi wa kila siku,”amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.
Mhe. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akiwakaribisha washiriki wa mafunzo ya Kanuni na Mbinu za Usuluhishi wa Migogoro kwa maafisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) hawapo pichani.

Aidha, Mhe. Dkt. Kihwelo alieleza kuwa Chuo kina jukumu la kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya sheria ili kuwa na uwezo wa kusuluhisha migogoro mbalimbali inayotokea kwenye Mamlaka au Taasisi mbalimbali na kwa kufanya hivyo itapunguza mrundikano wa mashauri mahakamani.

Wakati huohuo Mjumbe wa Bodi na mshiriki wa mafunzo hayo, Bw. Fadhili Manongi ameelezea kwamba mafunzo haya yatawasaidia sana katika utoaji wa maamuzi na kuweza kutenda haki pamoja na kutoa ushauri wa nini kifanyike kuhusiana na migogoro watakayokutana nayo.
Bw. Fadhili ametoa ushauri kwa Mamlaka zote zinazofanya uthibiti, kuja Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kupata mafunzo kama haya.

Mafunzo hayo yamejumuisha maafisa wa EWURA wa ngazi mbalimbali ambao ni Wajumbe wa Bodi na wajumbe wa menejimenti.
Washiriki wa mafunzo ya Kanuni na Mbinu za Usuluhishi wa Migogoro kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) wakiwa wanafuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo kutoka kwa Mhe. Mohamed Chande Othman (hayupo pichani).
Mhe. Mohamed Chande Othman Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Kanuni na Mbinu za Usuluhishi wa Migogoro kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Mada mbalimbali zitawasilishwa na wawezeshaji mahiri na wabobezi katika masuala ya mbinu za usuluhisi wa migogoro ambao ni Mhe. Mohamed Chande Othman Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustin Kihwelo Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Robert V. Makaramba Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mhe. Rose Teemba Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news