Kinara wa utapeli Dar ni miongoni mwa wahalifu 91 waliodakwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi hilo limewanasa watuhumiwa 91 wanaojihusisha na makosa ya wizi na unyang’anyi wa magari na kusafirisha na kuuza dawa za kulevya.
Kamanda Muliro ameyasema hayo leo Januari 20,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akisisitiza kuwa,watuhumiwa wengine walionaswa kwenye operesheni hiyo ni matapeli wanaojifanya maafisa wa Serikali.

Pia amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni mafanikio ya operesheni waliyofanya tangu Januari Mosi hadi 12, 2022.

“Januari huwa kuna tabia ya watu kudai kwamba ni ngumu, hivyo baadhi ya watu wanajikita kwenye vitendo vya kufanya uhalifu bila kutambua kuwa jeshi limekuwa na operesheni kali dhidi ya watu wanaopanga njama kuhakikisha wanakamatwa na kuingizwa kwenye mifumo ya kisheria ili haki itendeke.Katika operasheni hiyo watuhumiwa 91 watapelekwa kwenye mifumo ya kisheria ili haki itendeke na mali tulizokamata zitaambatanishwa kwenye vielelezo vya ushahidi mahakamani,”amesema. 

Amefafanua kuwa, katika operesheni hiyo pikipiki zaidi ya 12 ambazo zilihusishwa na watuhumiwa wa unyang’anyi wa kutumia nguvu kwa kujifanya wanakodi pikipiki na kuwapeleka maeneo ambayo yako mbali na makazi ya watu na baadae abiria kugeuka mualifu zimekamatwa.

“Matapeli wengine tuliowakamata ni wale wanaojifanya maofisa wa serikali na wanapita kwenye ofisini kuwatapeli watu kwamba wanaweza kuwafanyia mipango mbalimbali ya kazi, lakini kuwachukulia fedha na kinara wao mmoja tumemkamata,”amesema.

Amesema, mali zingine walizonasa kupitia operesheni hiyo ni pamoja na vifaa vya majumbani ikiwame majenereta,televisheni na redio ambavyo vitapelekwa kama sehemu ya vielelezo vitakavyosaidia upelelezi mahakamani.

Wakati huo huo, jeshi hilo limesema kuwa, halitasita kutumia mifumo yake ya kiutendaji kufuatilia kwa siri ikiwemo kushirikiana na wananchi wema kuhakikisha watuhumiwa wanaopanga njama za kufanya uhalifu wanakamatwa kabla ya kutenda vitendo hivyo mahali popote. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news