Makachero saba mahakamani kwa tuhuma za kufanya mauaji

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Mtwara limewakamata na kuwafikisha mahakamani Maafisa wa Polisi saba kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kijana Mussa Hamisi Hamisi (25) mkazi wa Kijiji cha Ruponda Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Mauaji hayo yamefanyika baada ya marehemu Mussa Hamisi kudai fedha zake shilingi Milioni 33,748,980 ambazo maafisa hao wanadaiwa kuzichukua kutoka kwa kijana huyo baada ya kumfanyia upekuzi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Marck Njera amesema mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 na mwili wa marehemu ulitupwa Kitongoji cha Majengo Kijiji cha Hiari wilaya ya Mtwara.

Maafisa wanaoshikiliwa ni Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje -Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango -Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu wa Polisi Msaidizi Nicholaus Kisinza -Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai mkoa wa Mtwara, Mkaguzi wa Polisi John Msuya Mganga- Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Juma Mbalu.Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.

Kamanda Mark Njera amesema mtuhumiwa mmoja kwenye mauaji hayo mrakibu msaidizi wa polisi Greyson Mahenge amejinyonga kwa dekio akiwa mahabusu katika kituo cha polisi Mtwara mjini.

Kufuatia tukio hilo kamanda Njera amelionya jeshi hilo mkoani Mtwara kuwa halitamfumbia macho askari yoyote atakayebainika kujihusisha au kutenda kosa atakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news