Makamu wa Rais afanya Utalii wa Ndani Gombe, fahamu kwa kina kuhusu hifadhi hii

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametembelea Hifadhi ya Taifa Gombe mkoani Kigoma na kupata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vya utalii hususani wanyama adimu aina ya Sokwe Mtu.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 28, 2022 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi -Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makamu wa Rais aliyeambatana na Mke wake Mama Mbonimpaye Mpango alipata wasaa wa kupanda mti pamoja na kuzungumza na watumishi wa Gombe.

Hifadhi ya Taifa Gombe

Kwa wa mujibu wa makala iliyoandaliwa hivi karibuni na Mhifadhi mwanafunzi,Victor Obadia Wilson kutoka Idara ya Wanyamapori Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) na kuhaririwa na Alphonce Msigwa ambaye ni Mwikolojia Hifadhi za Taifa Tanzania,imebainisha kuwa, Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni miongoni mwa hifadhi kongwe hapa nchini Tanzania.

Hii ni hifadhi iliyosheheni vivutio mbalimbali vinavyobeba umaarufu wake. Licha ya uwepo wa hifadhi nyingine kama Mahale na Mto ugalla zenye wanyama jamii ya sokwe, lakini bado Hifadhi ya Taifa ya Gombe imezidi kushika hatamu kwa muda mrefu kutokana na upekee wa sokwe wanaopatikana katika hifadhi hii.

Hifadhi ya Gombe ina ukubwa wa kilomita za mraba 52 na inapatikana katika Mkoa wa Kigoma, Magharibi mwa Tanzania ikiwa ni sehemu ya milima iliyosheheni misitu minene inayotengeneza ikolojia nzuri katika hifadhi hii.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango akipanda mti ikiwa ni ishara ya hamasa ya kila mmoja kupanda miti ili kulinda hifadhi, mazingira na misitu yetu. (Na Mpigapicha Maalum).

Wanyama hawa jamii ya sokwe wanapenda kuishi maeneo ya misitu hivyo uharibifu wa misitu unaweza kuhatarisha maisha yao. 

Hifadhi hii inapatikana kando kando ya ziwa Tanganyika na uwepo wa ziwa hili umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza hadhi ya Hifadhi ya Gombe ambapo licha ya watalii kufurahia maajabu ya sokwe wanaopatikana katika hifadhi hii anaweza pia kufanya utalii kwa njia ya boti ( boating safari).

Mnamo mwaka 1943 Gombe ilianzishwa kama pori tengefu yaani Game reserve na mwaka 1968 ilipandishwa hadhi na kuwa hifadhi ya Taifa. 

Hifadhi hii imejipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na uwepo wa wanyama aina ya sokwe (chimpanzee) wanaoifanya hifadhi hii kujulikana kote ulimwenguni na kuwa kitovu cha utalii na kupelekea kuwa na mchango mkubwaa katika pato la taifa kwa kipindi kirefu.

Uhifadhi wa sokwe hawa katika Hifadhi ya Gombe umekuwa na mchango mkubwa hasa kwa kutoa fursa mbalimbali za kufanya tafiti ambapo watafiti kutoka pande zote za Dunia hufika katika hifadhi hii ya Gombe katika kutekeleza majukumu yao ya kiutafiti hasa kuhusu sokwe na maisha yao.

Dkt.Jane Goodall ni miongoni mwa watafiti kutoka ughaibuni waliosafiri na kufika katika eneo hili mnamo mwaka 1960 na kuanza kufanya utafiti wake uliohusu sokwe. 

Katika muktadha huo, tafiti hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa serikali yetu hasa katika kutatua changamoto zinazohatarisha maisha ya sokwe pamoja na kutoa njia bora za utunzaji wa sokwe ili wasitoweke.

Kwanini wanaitwa sokwe mtu?

Mara nyingi tunapenda kuwaita wanyama hawa sokwe mtu pasipo kujua sababu za mnyama huyo kuitwa hivyo. 
Hii ni kutokana na dhana mbili zinazoelezea binadamu ( mtu) katika uasili wake ambapo kuna dhana ya kidini, uumbaji ( creation theory) na dhana ya kisayansi ( evolution theory) ambapo dhana hii ya kisayansi inaelezea jinsi ambavyo binadamu alibadilika kutokana na mnyama sokwe katika vipindi mbali mbali pamoja na sababu za mazingira na kuwa binadamu wa sasa.

Hivyo, kutokana na dhana hii inaonyesha dhahiri kuwa sababu ya sokwe kuitwa sokwe mtu ni kuwa na baadhi ya sifa zinazoendana na zile za binadamu. 

Kitu cha kushangaza kwa wanyama hawa huishi katika familia zao ( baba,mama na watoto) kwa pamoja pia wanao uwezo mkubwa wa kutambuana sokwe wa familia moja na mara nyingi huishi kwa upendo na furaha isiyokifani.

Sokwe hubeba mimba na kuzaa kama ilivo kwa binadamu na mtoto anapozaliwa hubebwa mgongoni kwa ajili ya usalama dhidi ya maadui na upendo wa mama kwa mtoto. 

Pamoja na hayo sokwe hawana mikia kama walivo nyani na ngedere na miili yao hufunikwa kwa manyoya meusi na huonekana wakitembea chini kwa miguu minne au juu ya miti na ni wanyama rafiki wenye uwezo wa kujamiiana ( social animals).

Upekee na maajabu ya sokwe wa Gombe

Sokwe wa Hifadhi ya Gombe wamekuwa wakibeba wasifu ambao umeitofautisha hifadhi hii na hifadhi nyingine hapa Tanzania ambapo taarifa za wanyama jamii ya sokwe zimewahi kuchapishwa na kituo Cha redio cha nchini Ujerumani DW kupitia Idhaa ya Kiswahili katika masuala ya kijamii mnamo tarehe 12,8,2014 ikimuelezea mwanasayansi na mtafiti aliyefika hifadhi hii ya Gombe, Dkt.Jane Goodall kutoka Uingereza na haya ni miongoni mwa maajabu ya sokwe hawa;
Sokwe wa Gombe ndio sokwe pekee Tanzania kufanyiwa utafiti kwa muda mrefu. Viumbe hawa wamefanyiwa utafiti takribani miongo mitano katika kufatilia mienendo na maisha yao.

Hufanyiwa ufatiliaji kila siku, hii ni pekee katika Hifadhi ya Gombe ambapo ufatiliaji huo umesaidia kujua mahali sokwe walipo katika hifadhi na shughuli wanazofanya.

Lakini pia, uwezekano wa kuwaona sokwe katika Hifadhi ya Gombe ni mkubwa ukilinganisha na hifadhi nyingine (huonekana kirahisi) na hii ni kutokana na ufuatiliaji mzuri.

Sokwe hawa huishi katika mazingira yao ya asili. Juhudi za utunzaji wa mazingira katika Hifadhi ya Gombe imeshika kasi hivyo kuwafanya sokwe hawa waishi katika ikolojia asilia ambayo haijaharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Fahamu taratibu za kuwatazama sokwe wa Hifadhi ya Gombe

Wageni wengi wanapotembelea Hifadhi ya Gombe huwa na shauku kubwa ya kuwaona sokwe,lakini katika kuhakikisha uhifadhi bora wa viumbe hawa pamoja na usalama, wageni hutakiwa kufuata taratibu zifuatazo;

Mosi, watalii hutakiwa kuwa umbali wa angalau mita kumi kutoka alipo sokwe ili kuepesha kuambukizana magonjwa mfano magonjwa ya mafua.

Pia unatakiwa kuvaa barakoa (mask) inayoziba mdomo na pua wakati unapo watazama sokwe hasa unapokohoa na kupiga chafya.

Tatu, hutakiwi kula au kunywa chochote unapowatazama sokwe.Nne, unatakiwa kutembea na vitu vyako au weka vitu vyako sehemu ambayo sokwe hawawezi kufika.

Tano, umri unaoruhusiwa kwa utalii wa sokwe ni kuanzia miaka 12. Wakati wa kupiga picha usitumie kamera inayotoa mwanga/flash.

Aidha, sokwe anapokukaribia hutakiwi kukimbia wala kupiga kelele, unashauriwa kurudi nyuma nyuma taratibu hii inamjengea mgeni uwezo wa kutengeneza urafiki sokwe.

Hifadhi ya Taifa ya Gombe inazidi kuingia katika kumbukumbu ya Dunia kutokana na uwepo wa wanyama wengine na kumpa nafasi mtalii kuwaona wanyama wengine wa jamii hii kama mbega mwekundu, nyani, tumbili na karasinga au kima. 

Wanyama hawa wote huongeza shauku ya kila mtalii kutamani kusalia katika hifadhi hii ya Gombe akifurahia mandhari safi na upepo mzuri unaovuma kutoka ziwa Tanganyika.

Licha ya umuhimu wa uwepo wa wanyama jamii ya sokwe katika Hifadhi ya Gombe, wanyama hawa wamekuwa wakikumbwa na changamoto za kiusalama hasa zinazohusiana na shughuli za kibinadamu kama uwindaji, kuongezeka kwa watu na makazi pamoja na shughuli za ukataji mkaa hivyo shughuli hizo zimekuwa zikiathiri makazi ya sokwe hawa.

Hata hivyo, kutoweka kwa sokwe kumekuwa kukihusianishwa na kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia ya nchi kutokana na kupotea kwa misitu. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa hifadhi hiyo. (Na Mpigapicha Maalum). 

Jamii ya kitanzania inashauriwa kuchukulia suala la uhifadhi wa sokwe kwa upekee wake kutokana na kuwa wanapatikana kwa uchache duniani ukilinganisha na wanyama wengine kama tembo, simba, nyati, swala na wengine wengi.

Post a Comment

0 Comments