Matokeo chanya ya vikao vya Muungano yampa faraja Rais Dkt.Mwinyi, afanya mazungumzo na Waziri Mkuu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika vikao vya Muungano ikiwa ni pamoja na kutatuliwa mambo kadhaa. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipofika Ikulu jijiji Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo Januari 8,2022.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa na kumpongeza kwa kumtembelea.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi kwa usimamizi mzuri wa vikao hivyo vya Muungano ambavyo vimeweza kuleta tija na kutatua mambo kadhaa ambapo kati ya hoja 18 tayari hoja 11 zimeshapatiwa ufumbuzi na kwa zile zilizobaki ufumbuzi wake utapatikana ndani ya muda mfupi ujao. 

Rais Dkt. Mwinyi ametoa salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri uliopo, hatua ambayo imekuwa na maslahi mazuri kwa pande zote mbili ikiwa ni pamoja na mgao wa fedha za mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), hatua ambayo itasaidia kujenga huduma za jamii pamoja na kuwapangia mipango wajasiriamali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa wakiangalia mandhari ya bahari, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Amesema kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa na msaada mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhika na hatua ya ushirikiano unavyokwenda hali ambayo itasaidia kuimarisha na kukuza uchumi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa shukurani kutokana na nchi kuwa na amani na utulivu na kusema kwamba hatua hiyo ndio inayopelekea kuimarika kwa uchumi na kueleza kwamba kwa upande wa Zanzibar, utulivu umeweza kupatikana na wananchi wanashirikiana vyema na hivi sasa kuna kila sababu ya kupiga hatua kimaendeleo.

Alieleza athari za UVIKO -19 zilivyoathiri uchumi wa Zanzibar na kueleza jinsi dalili za kuongezeka kwa watalii na kueleza haja ya Zanzibar kujifunza katika ukusanyaji wa mapato hasa baada ya janga hilo la maradhi kutokana na uchumi wa Zanzibar kuwa tegemezi kwa utalii.

Naye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa kupata fursa ya kuiongoza Zanzibar hali ambayo anastahili na ameanza vizuri kuongoza kwani nchi imetulia na uhusiano wa Wazanzibari umezidi kuimarika.

Amepongeza jinsi Rais Dkt. Miwnyi wanavyoshirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan na kuahidi kwa upande wao wasaidizi wataendelea kupokea maelekezo yao na kusimamia majukumu ya kuwatumia Watazania wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa jitihada zake za kuimarisha uchumi na hasa katika kuitumia fursa ya Uchumi wa Buluu ambao ni uchumi wa Buluu na kuweka nguvu katika uchumi huo na kueleza kwamba kwa upande wa Tanzania Bara nayo itapanua wigo kutokana na Sera hiyo aliyoiweka Dkt. Mwinyi katika uchumi. 

Waziri Majaliwa amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha vikao vya Muungano vinaleta tija na kuweza kuondoa changamoto zilizopo kwa haraka.

Amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba mamla za ukusanyaji wa kodi zitahakikisha zinakusanya kodi bila ya kutumia nguvu kwa lengo la kuwajengea imani Watanzania kwa Serikali yao pamoja na kuwaamini viongozi wao wote ili nchi izidi kupata mafanikio.

Mapema, Rais Dkt. Mwinyi alifanya mazungumzo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anayeshughulikia Masuala ya Watu wenye Ulemavu Ummy Khamis Nderiananga Ikulu Zanzibar na kueleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inawasaidia watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwajenga vyuo vya amali Unguja na Pemba ili wapate elimu za stadi za maisha. 
Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza kwamba unapotaka kumuwezesha mtu ni vyema ukampa elimu kwanza ili iweze kumsaidia katika kuendesha shughuli zake na ndio maana Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ya kutaka kuwajengea vyuo wajasiriamali.

Katika maelezo hayo Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza kwamba Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itafanya kila iwezekanavyo katika kuhakikisha inawasaidia na inawaunga mkono watu wenye ulemavu.

Alieleza hatua na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais pamoja na Wizara ya Afya katika kuwawekea mazingira mazuri na kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Alibainisha kwamba, miongoni mwa mikakati na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwasaidia watu wenye ulemavu ni kuhakikisha fedha za mkopo wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo wajasiriamali watasaidiwa pia, watu wenye ulemavu nao watafaidika na fedha hizo ili kuwaondoa katika dimbwi la umasikini.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameleza uwepo wa watu wenye ulemavu ndani ya Serikalini na kusisitiza haja ya kuongezeka kwa idadi yao huku akieleza kwamba wazo la kuwasaidia watu wenye ulemavu mmoja mmoja nalo litafanyiwa kazi ili mafanikio yaweze kupatikana kama vile yalivyopatikana kwa upande wa Tanzania Bara.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Naibu Waziri Ummi Nderiananga kwa ziara yake aliyoifanya Unguja na Pemba sambamba na kuendeleza mashirikiano zaidi kati ya Serikali zote mbili hasa katika wakati huu wa shamrashamra za miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964.

Nae Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Anayeshughulikia Masuala ya Watu wenye Ulemavu Ummy Khamis Nderiananga alieleza salamu za watu wenye ulemavu alizopewa ili azifikishe kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Alitoa pongezi kwa hatua za uteuzi ambazo amezifanya Rais Dkt. Mwinyi kwa watu wenye ulemavu ambapo pia, wakuu wa Mikoa nao wamemuunga mkono juhudi hizo kwa kuwateua Masheha ambao ni watu wenye ulemavu huku akieleza kwamba Serikali zote mbili zilivyoweka mikakati ya kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Aidha, Naibu Waziri Ummi Nderiananga alieleza mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akieleza jinsi alivyofanya ziara yake Unguja na Pemba kuanzia tarehe 3 mwezi huu hadi tarehe 7 pamoja na kutoa misaada mbalimbali kwa watu wenye ulemavu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news