MHESHIMIWA KIJAZI AWAASA WAFANYAKAZI WA TANAPA KUIMARISHA MSHIKAMANO

NA MWANDISHI MAALUM

ALIYEKUWA Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amewataka wafanyakazi wa TANAPA kuendeleza umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya shirika.
Ametoa wito huo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa Kamishna wa Uhifadhi mpya William Mwakilema. 

“Mafanikio yaliyofikiwa kwa upande wa TANAPA yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kuimarisha mshikamano,"amesema Mheshimiwa Kijazi.
Ameielekeza TANAPA kuongeza bidii katika kuyatekeleza majukumu ya msingi ambayo ni kuendeleza uhifadhi na utalii. Alitahadharisha kuwepo kwa dalili za ujangili katika hifadhi zetu na kusisitiza kuzilinda maliasili hizi kwa nguvu zote.

Kuhusu utalii, amesisitiza kuongeza bidii ili kuwavutia watalii wa ndani na nje. 

"Ili kufikia lengo hili ni lazima kuboresha miundombinu, kutoa huduma bora kwa watalii na kuendelea kuvitangaza vivutio vyetu,"amesema.
Naye Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema ametoa shukrani zake za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kushika nafasi hiyo na kuahidi kutekeleza kazi  kwa dhati na bila upendeleo, chuki wala majungu. 

Amewataka watumishi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuendelea kulinda tuzo mbalimbali zilizopatikana hasa za ESQR na ISO.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news