Rais Dkt.Mwinyi afungua mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano

NA MWANDISHI DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi kwa wawekezaji waliowekeza katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kuwa na ushirikiano wa karibu na jamii inayowazunguka katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii, hususani katika sekta za afya, elimu na huduma za maji safi na salama. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kushoto) akiondoa kitambaa kufungua Hoteli ya Marijani Resort &Spa katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja leo. (Picha na Ikulu). 

Dkt. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo Januari 6,2022 katika hafla ya Ufunguzi wa Mradi wa Hoteli ya Kitalii ya Nyota Tano ya Marijani Resort & SPA iliyopo Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

Amesema, moja ya njia ya kujenga uhusiano mwema kati ya wawekezaji na wananchi ni kujenga utamaduni wa kurejesha sehemu ya faida wanayopata kwa jamii ili kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii. 

Ameeleza kuwa, kuna baadhi ya maeneo ambapo wawekezaji wamekuwa hawana ushirikiano na wadau mbalimbali wa utalii kama vile wavuvi,hivyo amesisitiza umuhimu wa kushirikiana ili pande zote ziweze kunufaika. 

Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumpongeza mwekezaji wa mradi huo kwa namna anavyoshirikiana na wananchi wa Pwani Mchangani katika kuendeleza kilimo cha zao la Mwani. 

Aidha, amesema kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya uwekaji wa mawe ya msingi pamoja na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya hoteli hapa nchini ni mafanikio ya juhudi za Serikali za kuvutia wawekezaji hapa nchini, ikiwa ni kielelezo cha kuvutiwa na sera na mipango iliopo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati)akikata utepe kama ishara ya Ufunguzi wa hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hafla iliyofanyika leo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja (wa tatu kulia) Mke wa Rais Mama Marium Mwinyi . (Picha na Ikulu). 

Amesema, juhudi za pamoja kati Serikali na wadau wa Utalii pamoja na kuwepo kwa mani na utulivu nchini, ni mambo yanayoendelea kuvutia Wawekezaji. 

Amesema, hatua hiyo imechochea Wawekezaji wengi kujenga azma ya kuja nchi kuwekeza katika Visiwa kumi vidogo vidogo katika miradi ya hadhi ya juu, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na kudumisha amani iliopo. 

Amempongeza, mwekezaji na wanahisa wenzake kutoka Mauritius ambao ni Kampuni za Avenes Limited, Harwood Limited na Amcop Investment Limited kwa uamuzi wao wa kuwekeza hapa nchini katika mradi mkubwa wenye hadhi unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 10.5, na akatumia fursa hiyo kuwahakikishia mitaji na amana zao kuwa salama. 

Aidha, akatumia fursa hiyo kuwahimiza wafanyakazi wote wanaotoa huduma kwa wawekezaji na wageni kuhakikisha wanatoa huduma zinazokidhi viwango na matarajio ya watalii kwa misingi ya uzalendo na uadilifu, kwa kutambua kuwa mafanikio yaliopo ndio msingi wa kukuza pato la taifa na kuimarisha ajira. 

Alisema katika kuimarisha Uwekezaji, Serikali inatekelezaji mikakati mbali mbali ya kuimarisha mazingira ya Uekezaji nchini, kwa kuimarisha miundombinu muhimu kwa maendeleo ya sekta ya Utalii. 

Alisema hatua za kuimarisha viwanda vya ndege na bandari ina lengo la kuimarisha sekta ya usafirishaji na akabainisha hatua iliyochukuliwa na serikali katika kukiimarisha kiwanda cha Ndege cha Pemba inalengo la kukifanya kisiwa hicho kuwa eneo maalum la Kimkakati na Uwekezaji. 

Alitoa wito kwa Wawekezaji katika sekta zote kuja kuwekeza Pemba, akisema kwamba kuna fursa nyingi na mazingira ya kuvutia. 

Aidha, Dkt.Mwinyi aligusia suala la usalama wa watalii na kusema ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali, hivyo akawahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kufanyakazi kwa karibu na Wawekezaji walio katika maeneo yao ili kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili. 

Aliitaka mikoa hiyo kuwa na mipango thabiti ya kupambana na vitendo vyote vinavyoweza kurudisha nyuma juhudi za kukuza utalii, kuharibu utamaduni pamoja na kuipa nchi sifa mbaya. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi (kushoto) wakifuatana na Mwekezaji Rahim Balu (katikati) pamoja na kupata maelezo wakati alipotembelea sehemu mbalimbali mara baada ya ufunguzi wa hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hafla iliyofanyika leo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja (kulia) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Kazi,Uchumi na Uwekezaji, Mhe.Mudrik Ramadhan Soraga.(Picha na Ikulu). 

Vile vile akazitaka taasisi zinazoshughulikia masuala ya ujasiriamali kuongeza kasi katika kubuni mipango itakayoweza kutumika ipasavyo katika sekta ya utalii ili kuimarisha soko la ndani la bidhaa zinazozalishwa nchini. 

“Bado hatujawaunganisha vizuri wajasiriamali wetu wa sekta ya utalii, kwenye eneo hili kuna fursa nyingi za wajasiariamali wetu,”amesema. 

Amewapongeza wamiliki wa hoteli hiyo kwa kuonyesha nia ya kununua bidhaa zote zinazopatikana hapa nchini, huku akiwakumbusha wawekezaji kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano yaliomo katika mikataba, ikiwemp kutii sheria za nchi katika ulipaji wa kodi na tozo mbali mbali , ajira pamoja na maslahi ya wafanyakazi wao. 

Nae,Waziri wa Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla na kupongeza juhudi na miongozo ya Rais Dkt. Mwinyi kuwa imekuwa chachu katika kuvutia wawekezaji. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi (kushoto) wakifuatana na Mwekezaji Rahim Balu (katikati) pamoja na viongozi wengine wakifuatana kabla ya kuagana baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguzi wa Hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika Kijiji cha Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.(Picha na Ikulu). 

Amesema, wizara hiyo inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora ya uwekezaji, hususan katika suala la utoaji wa maamuzi ili kuyatolea maamuzi ya haraka mambo mbalimbali. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahamoud amesema katika kufanikisha dhamira ya kupunguza ajali na kuimarisha usalama wa watali, mkoa huo unaendelea na programu maalum ya kuzungumza na madereva wa aina mbalimbali ikiwemo wanaoendesha gari za watalii, baada ya kubaini kuwepo matukio ya ajali za mara kwa mara zinazojitokeza mkoani humo. 

Alieleza kuwa, Mradi wa Marijan Resort & SPA unatoa funzo kwa kiasi gani wawekezaji hao wanaweza kuendesha shughuli zao za kitalii kwa mashirikiano makubwa na wakulima wa mwani, ambao ni sehemu kubwa ya wananchi wa maeneo hayo. 

Mapema, Mwenyekiti wa Kampuni ya ZK Venture Ltd, Wawekezaji wa Mradi wa Marijani Resort & SPA, Amin Manji amesema, ujio wa mradi huo unatokana na ari na juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi za kuvutia Wawekezaji kote Duniani kuja kuwekeza Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakipata maelezo kutoka kwa Mwekezaji Rahim Balu baada ya ufunguzi wa hoteli ya Marijani Resort &Spa ikiwa ni katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, hafla iliyofanyika leo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja (wa tatu kulia). (Picha na Ikulu). 

Amesema, Mradi wa Marijani Resort & SPA ni mradi wa hoteli ya nyota tano, uliofanikishwa ujenzi wake kupitia kampuni mbalimbali za kizalendo, ukiwa na jumla ya vyumba 82 na maeneo mbalimbali ya utoaji huduma pamoja na kuwa na uwezo wa kuchukua wageni 104. 

Katika hatua nyingine, mwananchi na mkulima wa mwani kutoka Shehiya ya Pwani Mchangani, Mwanakheri Mussa Mohamed alimshukuru mwekezaji wa mradi huo kwa kuonyesha imani ya dhati kwa wananchi wa maeneo hayo na kusema ni mfano mzuri wa kuigwa na wawekezaji wengine. 

Amempongeza, mwekezaji huyo kwa kutoa fursa kwa wakulima wa mwani kuendelea na shughuli za kilimo hicho katika maeneo yao ya asili (mbele ya hoteli) pamoja na kuwapatia eneo maalum kwa ajili ya kuanikia mwani huo. 

Pia ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia namna ya kuwainua wakulima wa kilimo hicho cha mwani, kwa kigezo cha kutozwa kiwango kidogo cha bei, ikilinganishwa na kazi ngumu ya kilimo hicho, sambamba na kuiomba Serikali kuwaondolea kero ya ukosefu wa maji safi na salama wananchi wa eneo hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news