RC Kunenge aguswa na uwekezaji mkubwa kiwanda cha marumaru, atoa wito

Na ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, Watanzania wanapaswa kujivunia na uwepo wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza marumaru (tiles) cha Twyford Ceramics (Keda) kwa kuwa bidhaa hizo zina ubora mkubwa kuliko zile zinazotoka nje ya nchi.
Kunenge amesema kiwanda cha Keda kilichopo Chalinze Wilayani Bagamoyo ndio kiwanda kikubwa kinachozalisha marumaru Afrika Mashariki na Kati na kwamba suala la kuagiza nje ni kupoteza muda.

Amesema hayo alipotembelea kiwandani hapo akiwa na timu ya wataalamu mbalimbali ambapo lengo la ziara hiyo ni kutaka kujua changamoto zinazowakabili ili zitatuliwe.

"Nimekuja kuona hali ya uzalishaji ya kiwanda hiki maana Serikali imefanya sehemu kubwa, lakini nataka kujua kama kuna mapungufu au changamoto ili nipate kusaidia,"amesema.

Amesema kuwa, Serikali imefanya kazi ya kumuwekea mazingira mazuri mwekezaji huyo na sasa anazalisha marumaru nzuri zenye ubora wa kiwango cha juu kwa hiyo ni wakati muafaka wa Watanzania kuona umuhimu wa kutumia bidhaa hiyo.
Aidha,Kunenge amesema haitakuwa na maana ya uwepo wa kiwanda hicho endapo watu watakimbilia kuagiza marumaru nje ya nchi wakati hapa nchini kwetu zipo tena za kiwango cha juu huku akisema kufanya hivyo ni kukosa uzalendo.

"Nipo kwenye ziara ya kutembelea viwanda vyote vikubwa vilivyopo ndani ya Mkoa wa Pwani, lakini nilipofika katika kiwanda hiki hakika nimefurahi kuona aina ya Marumaru zinazozalishwa hapa kwakuwa zina ubora mkubwa,"amesema.

Amesema, Rais Samia ametengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji wa viwanda kwa lengo la kupanua wigo wa ajira kwa vijana pamoja na kuongeza mapato ya Taifa na kwamba malengo hayo yatafikiwa endapo wananchi wataunga mkono juhudi hizo.
"Kiwanda hiki wananchi wanapata marumaru bora, ajira kwa vijana na hata kutoa huduma za jamii,kwa hiyo lazima Serikali ihakikishe kiwanda hiki kinaendelea kwa faida za mwekezaji na Taifa letu,"amesema. 

"Tuwe wazalendo wa kupenda vya kwetu tusisubiri kuambiwa,dunia nzima inakijua kiwanda hiki na ubora wa bidhaa zake kwahiyo tutumie fursa tuliyonayo kwa kuhakikisha tunanunua bidhaa hizi,"ameongeza Kunenge.

Meneja wa kiwanda hicho, Bruce Ni amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutembelea kiwandani hapo kwakuwa inakuwa fursa kueleza changamoto zilizopo katika kiwanda chake.

Amesema,licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa lakini kwa sasa anamshukuru Rais kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kwa kuwa wanafanya shughuli zao bila usumbufu.
Meneja Ni ameiomba Serikali iendelee kuwasaidia katika kuboresha miundombinu ya maji,pamoja na umeme kwa kuwa umeme wanaoupata ni mdogo na hautoshelezi katika mahitaji yao ya kila siku.

Hata hivyo,ameiomba pia miradi ya mikubwa ya Serikali itumie bidhaa zake katika utekelezaji wake kwani itakuwa njia sahihi ya kuendeleza kiwanda hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news