TFRA na juhudi za kutatua kero ya mbolea kwa wakulima

 NA NURU MWASAMPETA-TFRA

IMEELEZWA kuwa, janga la ugonjwa wa Uviko-19 lililoikumba Dunia mwishoni mwa mwaka 2019 limesababisha athari nyingi kwa uchumi wa nchi mbalimbali duniani, ambapo athari hizo zimejidhihirisha katika Sekta ya Mbolea.

Hali hiyo imechangia bei ya mbolea kwenye soko la Dunia kupanda na kusababisha changamoto ya bei kwa wakulima nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Joseph Charos (wa kwanza kushoto-mbele) akiwakaribisha wafanyabiashara na baadhi ya watumishi wa TFRA kwenye kikao kilicholenga kupokea mapendekezo ya kuboresha suala la upatikanaji wa mbolea kwa wakulima nchini. (Picha na TFRA). 

Katika kuhakikisha tatizo la upatikanaji na bei ya mbolea nchini linadhibitiwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika viwanda vya mbolea na kwa viwanda vilivyopo ambavyo uzalishaji wake ni mdogo hususani vinavyozalisha mbolea ya maji vimeendelea kuboreshwa kwa kupanua maeneo ya uzalishaji, kufunga mashine na miundombinu mingine katika viwanda hivyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima. 

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Joseph Charos alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia mwezi Julai mpaka Desemba 2021. 

Aidha, Charos alibainisha kuwa maendeleo ya viwanda vya mbolea kwa ujumla ni mzuri kwani viwanda vilivyopo vimeendelea na uzalishaji ambapo kwa kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 TFRA imekuwa na jukumu la kuhamasisha matumizi ya mbolea zinazozalishwa ndani ya nchi kwa wakulima.
Kaimu Meneja wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Elizabeth Bolle akizungumza wakati wa kikao baina ya TFRA na wafanyabiashara wa mbolea ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ya kuitaka TFRA kukusanya maoni yatakayosaidia kuondoa kero ya mbolea kwa wakulima nchini. (Picha na TFRA).

Pamoja na hayo, Charos alibainisha kuwa, maendeleo ya wawekezaji wapya walioonesha nia ya kuwekeza na walioanza ujenzi wa viwanda vya mbolea nchini wanaendelea vizuri. Anasema ujenzi wa kiwanda cha Mabwepande Composite Manure umekamilka na uzalishaji wa mbolea kwa ajili ya majaribio unaendelea . 

Aliongeza kuwa, ujenzi wa kiwanda kipya cha mbolea cha Itracom kinachojengwa Jijini Dodoma na mwekezaji fertilizer limited kipo katika hatua mbalimbali za ujenzi ikiwemo uzio, majengo ya ofisi, maghala na majengo ya kiwanda, ujenzi huo umefikia asilimia 57%, aidha mitambo ya kuzalishia mbolea iliyowasili katika eneo la kiwanda umefikia asilimia 68%. 
Wajumbe wakisikiliza kilichokuwa kikizungumzwa na Kaimu Meneja wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Elizabeth Bolle (hayupo pichani) wakati wa kikao kilichofanyika hivi karibuni baina ya TFRA na wafanyabiashara wa mbolea nchini. (Picha na TFRA). 

Aliongeza kuwa, katika kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/2022 kuna wazalishaji walioonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea ya asili kwa kutumia majani na wadudu, na kubainisha kuwa wazalishaji hao wapo mikoa ya Morogoro na Mbeya ambapo tayari wameanza uzalishaji wa mbolea ya majaribio na wanaendelea na taratibu za usajili wa mbolea hizo.

Hizi ni baadhi ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za wananchi wake hususani wakuliama ambapo asilimia 68 ya watanzania wameajiriwa katika sekta hiyo muhimu ya kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news