Stephen Masele ajitosa mchakato wa kumrithi Ndugai nafasi ya Uspika

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Stephen Julius Masele leo Januari 10 amechukua fomu ya kugombea Kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Masele ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Kwa za wa Bunge la Afrika (PAP) amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge leo katika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es salaam.

Amefikia uamuzi huo, ikiwa tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanza mchakato wa kumsaka mrithi wa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ambaye alijiuzulu Januari 6, mwaka huu.

Katibu wa NEC- Itikadi Uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka, Januari 9, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Zanzibar alisema mchakato huo utaanza kuanzia tarehe 10 hadi 30 Januari,mwaka huu.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya Ndugai kuandika barua kwa hiari yake na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM jijini Dodoma.

Alisema kufuatia hilo CCM inawatangazia wanachama wake wote kwamba utaratibu wa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea atakayechaguliwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujaza nafasi ys Spika wa Bunge.

Shaka alisema utaratibu huo ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayotambua Spika kuwa ndio kiongozi mkuu wa Bunge na nafasi hiyo haiwezi kuwa wazi na Bunge likaendelea kufanya shughuli zake.

Akinukuu Katiba hiyo alisema; Ibara ya 84 (i) kutakuwa na Spika ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni wabunge au wenye sifa za kuwa wabunge, atakuwa ndio kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge.

“Ibara ya 84(viii) inasema hakuna shughuli yoyote itakayotekelezwa katika Bunge isipokuwa uchaguzi wa spika wakati wowote ambao kiti cha spika kipo wazi.

“Ibara ya 86(i) kimeeleza kutakuwa na uchaguzi wa spika katika kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya, na katika kikao cha kwanza chochote mara baada ya kutokea kiti cha spika kuwa wazi.

“Kwa minajili hiyo, katika kutekeleza matakwa ya kikatiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, nichukue fursa hii kwa niaba ya chama kutangaza kwamba mchakato wa kujaza kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utatekelezwa kwa ratiba ifuatayo sambamba na vikao vya mchujo na uchaguzi wa wabunge wa CCM kabla ya kupelekwa bungeni kuendelea na utaratibu mwingine,” alisema.

Alisema kuanzia tarehe 10 hadi 15 zoezi la kuchukua fomu litaanza rasmi na tarehe 15 ifikapo alasiri zoezi hilo litakuwa limekamilika.

Alisema wale wenye sifa alizotaja wanakaribishwa kuchukua fomu katika makao makuu ya chama ofisi kuu, makao ya chama Dodoma, ofisi ndogo Dar es salaam au Kisiwandui wakifika watapata maelekezo namna ya kuchukua fomu hizo.

Alisema Januari 17, 2022 Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashuri Kuu ya Taifa juu ya wagombea ambao wamejitokeza kuomba kiti hicho cha uspika.

“Tarehe 18 hadi 19 Januari kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho ambapo Kamati kuu ya Halmashauri Kuu itafanya kazi hiyo kwa eneo ambalo litaelekezwa.

“Kuanzia tarehe 21 hadi 30 Januari katika siku hizo, cocus ya chama ya wabunge wa CCM itapiga kura kumpata mgombea ambaye atakwenda bungeni kuomba kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania,” alisema.

“Nichukue fursa hii kuwataka watanzania wote ambao wanakidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na CCM, kutambua kuwa wana nafasi na wana fursa ya kujaza nafasi hii,” alisema Shaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news