Tume ya Madini yaagizwa kutafuta masoko

NA STEVEN NYAMITI-WM

NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wakubwa wa madini ya Vito ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wachimbaji wa madini kupata masoko.
Hayo yameelezwa alipotembelea machimbo ya migodi ya Vito (Ruby) katika Kata ya Mundarara wilayani Longido Mkoa wa Arusha.

Agizo hilo, amelitoa alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo katika eneo hilo baada ya kupokea malalamiko ya wachimbaji hao kukosa soko la uhakika la Madini aina ya Vito hususan yenye ubora wa kati na hafifu (Semi Gem/Cheapstone) yanayopatikana kwa wingi katika mkoa wa Arusha. 
Pia, aliendelea kusema Serikali imebaini wapo watu wanafanya shughuli za uchimbaji madini ambao hawapo kwenye mfumo rasmi na hawana leseni wala kitalu lakini wanajishughilisha na masuala ya madini kiholela na kupelekea hasara kwa Taifa.

Vile vile, alisema Serikali ipo kwenye hatua ya kutambua aina ya Madini yote yanayochimbwa nchini katika maeneo mbalimbali pamoja na kubaini maeneo mapya yenye madini ili Serikali inufaike, amesema taasisi zipo mbili, GST hupima juu ya Ardhi na kubaini madini yaliyopo pamoja na STAMICO wanaofanya tafiti za nadini kwa kwenda chini zaidi.

Naye, Kamishina wa Madini, Dkt Abdulrahman Mwanga amesema miradi ya kimkakati ni muhimu ili wananchi waweze kunufaika na huduma za kijamii, hivyo amewataka wawekezaji hao kujitahidi kushirikiana na wananchi katika kutekeleza miradi mbalimbali.
"Wawekezaji wanapaswa kutekeleza wajibu na matakwa ya Sheria katika kuendeleza maeneo yao ili kupunguza migogoro inayojitokeza na Wananchi"alisema Dkt Mwanga

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurudin Babu aliwaasa wachimbaji hao kufanya kazi kwa kushirikiana na kuepuka mikwaruzano,na matatizo yatakayojitokeza ni vyema yakatolewa taarifa kwake kabla hayajafika kwa Naibu Waziri.

Ofisa Madini Mkoa wa Arusha, Mhandisi Alphonce Rikulamchu amesema uwepo wa madini aina mbalimbali katika wilaya ya Longido ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa wilaya na Watanzania wote kwa ujumla.

Mhandidsi Rikulamchu ametoa wito kwa wachimbaji , wafanyabiashara ya madini na wadau wote kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu ili kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato stahiki ya Serikali.

Mmiliki wa Kampuni ya Sendeu Agrovet Co. Ltd inayomilikiwa na mwekezaji mzawa Gabriel Sendeu alisema kazi ya uzalishaji inaendelea katika mgodi huo na kueleza kuwa mgodi huu kwa Sasa ni kitovu cha mapato ya Serikali.
"Kampuni yetu imekuwa ikisaidia miaka yote kusomesha watoto yatima, hii ni baraka naomba na wengine wenye uwezo tusaidie watoto hao waliopo ndani ya jamii,"alidai Sendeu.

Wilaya ya Longido ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Arusha iliyojaliwa kuwa na madini ya Vito (Ruby, Spessartite, Sunstone na Quartz) katika maeneo ya Sinonik, Kimwati na Mundarara pamoja na Madini ujenzi mchanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news