Neelkanth Salt Limited wafichua siri namna Serikali ya Awamu ya Sita ilivyowapa nguvu ya kuwekeza,RC Kunenge asisitiza jambo

NA ROTARY HAULE

KIWANDA cha Chumvi cha Neelkanth Salt Limited kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani kimeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwatatulia changamoto ya umeme iliyokuwa ikiwakabili kiwandani hapo muda mrefu.
Afisa RasIlimaliwatu wa Kiwanda hicho, Said Kubenea ametoa pongezi hizo mbele ya Mkoa wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge aliyetembelea kiwandani hapo kwa ajili ya kujionea shughuli za uzalishaji na changamoto zinazowakabili.

Akiwa kiwandani hapo Kunenge alikutana na uongozi wa kiwanda akiwemo Kubenea ambapo alielezwa juu ya changamoto ya umeme iliyokuwa ikiwakabili na kusema kwa sasa wamefurahi baada ya kuona jambo hilo limeshughulikiwa.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa sisi tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuwekea mazingira mazuri ya uzalishaji kwa kuwa hapo awali tulikuwa tunahangaika na suala la umeme, lakini baada ya kuingia Rais huyu madarakani jambo hilo limefanyiwa kazi na sasa limefikia asilimia 80,"amesema.
Amesema,awali walikuwa wanatumia diseli lita 1,000 kwa siku jambo ambalo lilikuwa linakwamisha uzalishaji, lakini baada ya kupata umeme huo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 200 mpaka kufikia tani 300 kwa siku.

"Tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani tumekuwa tukipata ushirikiano mkubwa kutoka taasisi zote za Kiserikali ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya na TANESCO pia, kwani mbali na kushughulikia umeme kiwandani hapa, lakini wametusaidia kupata umeme katika shamba letu la chumvi lililopo Shungubweni,"amesema Kubenea.

Kubenea ameongeza kuwa, kiwanda chao kimefanikiwa kuajiri jumla ya wafanyakazi 920 wengi wao wanatoka katika maeneo ya Mkuranga na Mkoa wa Pwani kiujumla ambapo ajira hizo zitaongezeka kulingana na mahitaji.

Kubenea amesema kuwa, kiwanda hicho kilifunguliwa mwaka 2017 huku kikiwa kinalipa kodi zote za kisheria za Serikali Kuu na Mitaa pamoja na kuwalipia watumishi kwenye mifuko ya Hifadhi ya jamii kama vile NSSF ,WCF na PAYE.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, kazi inayofanywa na kiwanda hicho ni kubwa na ndio maana Serikali imewafuata ili kupata changamoto zake na kuona namna ya kusaidia.

Kunenge amesema, Serikali ya Rais Samia imejipanga na imedhamiria kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kusudi wanapozalisha pande zote ziweze kunufaika kwa mapato.

"Nimepita katika maeneo yote ya uzalishaji wa kiwanda hiki,nimeona Chumvi inayozalishwaji ipo katika mazingira mazuri lakini kikubwa zaidi ile changamoto ya umeme sasa imemalizika ndio maana hata uzalishaji umeongezeka kutoka tani 200 mpaka 300,haya ndio matunda ya kazi ya Rais Samia,"amesema Kunenge.l
Kunenge amesema, kiwanda hicho ni kikubwa na chumvi wanayozalisha inatumika katika Nchi za Afrika Mashariki,Nchi za Ukanda wa SADC pamoja na nchi nyingine duniani kwani lazima Watanzania nao wahakikishe wanatumia chumvi hiyo kwa kuwa ni bora na salama.

"Nimeona mazingira ya usalama wa chumvi hii na hata katika kuweka madini joto kwa hiyo sina mashaka zaidi ya kuwaomba Watanzania waunge mkono bidhaa zinazozalishwa katika nchi yetu ili kuwapa wawekezaji nguvu ya uzalishaji zaidi," amesema Kunenge.

Kunenge,amesema Serikali ya Rais Samia itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hasa katika kusimamia na kutatua changamoto zao huku akitoa wito kwa jamii kufanyakazi ya uzalishaji wa Chumvi kwakuwa hakuna sababu ya kuhangika wakati fursa hipo na soko la Chumvi lipo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Hadija Ally, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara ya kutembelea viwanda vilivyopo Wilayani humo huku akisema kiwanda cha Neelkanth licha ya uzalishaji wake lakini wamekuwa na msaada mkubwa kwa jamii.

Hadija amesema kiwanda hicho kimetoa msaada wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitumbo iliyopo Kata ya Mkuranga,ukarabati Shule ya Msingi Kiguza,viti,mabati kwa Shule ya Sekondari Shungubweni , ujenzi wa Zahanati pamoja na huduma nyingine za kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news