Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) yavutia wananchi wengi Zanzibar

NA MWANDISHI MAALUM

BANDA la Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) limeendelea kuwavutia wananchi wengi kutoka kila kona ya jiji la Zanzibar ambao wanajitokeza kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na mionzi nchini 
Hayo yamejiri wakati Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ikiendelea na jukumu la utoaji elimu juu ya majukumu inayoyatekeleza kisheria hapa nchini,kwenye Maonesho ya Mapinduzi yanayoendelea Viwanja vya Maisara jijini Zanzibar. 

TAEC ikiongozwa na kauli mbiu ya "Mionzi kwa Matumizi Salama na Teknolojia ya Nyuklia kwa Maendeleo ya Taifa". Watumishi wake wamekuwa mstari wa mbele kuwasikiliza wananchi mbalimbali na kujibu maswali yao kadri yanavyojitokeza, hali ambayo imewafanya wengi wao kutoa pongezi kwa huduma bora na ukarimu wa hali ya juu.
Dkt. Suleiman Suleiman ambaye ni Mtafiti Mwandamizi wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, akitoa Elimu kwa Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Shuwekha Khalfan alipotembelea Banda la TAEC, kwenye Maonesho ya 58 ya Mapinduzi, yanayoendelea Viwanja vya Maisara jijini Zanzibar.

TAEC iliundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003).Sheria ya Bunge Na. 7(2003) ilifuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).

Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Ni kutokana na ukweli kwamba, teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, kilimo, ufugaji, viwanda, maji na utafiti.

TAEC imepewa jukumu la kupima mionzi kutokana na sababu mbalimbali, kwani licha ya kuwa na faida nyingi za mionzi, isipotumika inavyotakiwa ni hatari ikiingia katika mnyororo wa chakula kwa sababu inatoa nishati toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile.

Kwa mujibu wa tume hiyo, viasili vya mionzi vinaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama. Hivyo, sababu kuu za kupima mionzi katika mnyororo wa chakula ni kuhakikisha chakula kinacholiwa na Watanzania hakina mionzi na hivyo kuwa salama kwa matumizi ya kawaida.

Pia ni muhimu kuhakikisha kuwa soko la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinalindwa ili kuzingatia ubora na viwango vilivyowekwa kulingana na miongozo na taratibu mbalimbali za Serikali.

Miongoni mwa sababu zinazosababisha upimaji wa mionzi ni kutokana na ukweli kuwa, usafirishaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking) unaweza kusababisha uchafuzi kwenye vyakula na mazingira.

Sababu nyingine kwa mujibu wa TAEC ni kuwepo kwa mionzi asili kwenye udongo na mazingira yetu kama vile madini ya urani katika maeneo mbalimbali nchini.

Post a Comment

0 Comments