MADIWANI MANISPAA YA MOROGORO WAJENGEWA UWEZO JUU YA MATUMIZI YA MFUMO WA MAEGESHO KIDIGITALI

NA ERICK MWANAKULYA-TARURA

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) leo Februari 10, 2022 umetoa mafunzo juu ya mfumo mpya wa ukusanyaji wa ushuru wa maegesho kwa njia ya kielektroniki kwa Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara, Maafisa Tarafa pamoja na Watendaji Kata Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro.
Mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa ushuru wa maegesho unatarajia kuanza kutumika mkoani Morogoro kuanzia Machi 1, 2022 ambapo mtumiaji wa maegesho atatakiwa kulipa Shilingi 300 kwa Saa na Shilingi 1,000 kwa Siku.

Mfumo wa Maegesho Kidigitali (TeRMIS) ni mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maegesho ya vyombo vya moto (parking fee), matumizi ya Hifadhi za barabara (Road Reserve User Charges) pamoja na Adhabu kutokana na Ukiukwaji wa matumizi ya hifadhi za barabara.
Mtumiaji wa maegesho atapaswa kulipia maegesho baada ya kupatiwa kumbukumbu namba ya malipo (control number) na atatumia Kumbukumbu namba hiyo kulipia maegesho kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala wa Huduma za fedha.

Mfumo huu wa Maegesho Kidigitali umetoa muda muafaka kwa mtumiaji wa maegesho kulipia maegesho ndani ya Siku 14 baada ya kutumia maegesho endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya Shilingi 10,000.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news