NHIF LINDENI UHAI WA MFUKO- WAZIRI UMMY

NA MWANDISHI MAALUM-NHIF

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetakiwa kuimarisha misingi ya kulinda uhai wake na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili waweze kunufaika na huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Makao Makuu ya Mfuko na kuzungumza na Menejimenti ya Mfuko juu ya utoaji wa huduma zake kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Nawapongeza kwa kazi na hakikisheni huduma zenu zinawafikia wananchi bila kikwazo chochote, hii ni Taasisi kubwa na dhamana yenu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha lakini ni muhimu pia kuhakikisha mnaulinda Mfuko na unakuwa endelevu". Alisema Mhe. Ummy.

Alisisitiza upanuaji wa wigo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili wawe kwenye utaratibu wa bima ya afya kwa kuwa ni muhimu kwa kila mtu. “Ongezeni jitihada ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua hii itasaidia sana wao kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu," alisema.
Akizungumzia huduma za ziada kwa wanachama na wananchi, aliutaka Mfuko kuweka utaratibu na kuzitangaza huduma hizo ili wananchi wapate elimu ya kutosha itakayowasaidia kufanya maamuzi ya kujiunga na kutumia huduma.

“Wekeni mikakati mbalimbali ya kuelimisha wananchi kuelewa dhana ya bima ya afya na kuona umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa usalama wa afya zao, tujue Mfuko huu una msaada mkubwa sana kwa wananchi hivyo toeni elimu na muwafikie wananchi huko waliko,” alisisitiza Mhe. Ummy.

Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri aliagiza uimarishwaji wa mifumo ya TEHAMA ili kuondoa mianya ya vitendo vya udanganyifu. Lakini pia kufanya uwekezaji wenye manufaa kwa Mfuko na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wakati. 
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mfuko Mkurugenzi Mkuu, Bw. Bernard Konga alimhakikishia Mhe. Waziri kuwa Mfuko umejipanga kuhakikisha unatoa huduma bora na kushughulikia changamoto zilizopo zikiwemo za masuala ya udanganyifu na kuongeza wigo wa wanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news