Polisi, Shirika la AMEND waja na mradi kabambe wa kufikisha elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi shule za msingi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la AMEND wamezindua mradi wa usalama barabarani kwa shule za msingi za Serikali jijini Dar es Salaam ujulikanao kama ‘Mahakama ya Watoto’ utakaohusisha utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa zaidi ya wanafunzi 11,000.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa (kushoto) akimkabidhi cheti cha ushirikiano bora wa usalama barabarani,Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali Tanzania la AMEND, Saimon Kalolo (kulia) wakati wa uzinduzi wa mradi wa usalama barabarani kwa shule za msingi za Serikali za jijini Dar es Salaam ujulikanao kama 'Mahakama ya Watoto'.Wengine wanaoshuhudia na maofisa wa polisi wa jeshi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 28,2022 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, SACP Wilbroad Mutafungwa amesema mradi huo utatoa kipaumbele kwa shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) linakadiria kuwa watu takriban 3,700 hufariki kila siku kwa ajali za barabarani duniani kote, huku Afrika ikiwa na idadi kubwa zaidi ya majeruhi watokanao na inaongezeka kila mwaka kutokana na kukua kwa kasi ya maendeleo.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Wilbroad Mutafungwa(katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Miradi wa 'Mahakama ya Watoto' ambao utakaohusisha utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa shule za msingi za Serikali za jijini Dar es Salaam.

“Nchini Tanzania takwimu zinaonesha kwa kipindi cha mwaka 2021, watu 1,245 walipoteza maisha na wengine 2,023 walijeruhiwa kutokana na ajali za barabarani. Taarifa zinaonesha kuwa jumla ya wanafunzi 56 walipoteza maisha na wengine 65 kujeruhiwa katika ajali hizo.

“Mwaka huu katika kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali nchini, Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani tukishirikiana na Amend tutaendesha mradi huu wa Mahakama ya Watoto...
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabara Wilbroad Mutafungwa( kushoto) akiwa anataka kumshika mkono Mkurugenzi wa Shirika la AMEND Simon Kalolo( kulia) baada ya kumkabidhi cheti cha Ushirikiano bora wa Usalama Barabarani leo Februari 28 mwaka 2022

"Ambao utahusisha kutoa elimu na mahojiano maalum ambayo yanafanywa kati ya wanafunzi na madereva watakaobainika kuvunja sheria za usalama barabarani kwenye maeneo ya shule hizo,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Aidha Kamanda Mutafungwa aliwataja waathirika wakuu wa ajali za barabarani kuwa ni watembea kwa miguu, waendesha pikipiki na bajaji, watoto wadogo wanaopandisha mshikaki kwenye pikipiki pamoja na madereva wa magari ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali Tanzania la Amend,Saimon Kalolo(katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa usalama barabarani kwa shule za msingi za Serikali za jijini Dar es Salaam ujulikanao kama 'Mahakama ya Watoto

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Amend, Simon Kalolo amefafanua mradi huo utahusisha shule 10 za Jiji la Dar es Salaam zenye uhitaji na kwamba mafunzo hayo yatawasaidia wanafunzi hao kutoa elimu ya usalama barabarani moja kwa moja kwa madereva.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa akiwa ameshika cheti cha Ushirikiano bora wa Usalama Barabarani na Mkurugenzi wa Shirika la AMEND nchini Tanzania Simon Kalolo.

"Na baada ya kukamilisha mradi huu tutatoa vyeti vya kuwatambua washiriki wote,” alisema Kalolo.Mradi wa namna hii ambao tunauzindua leo ulishawahi kutekelezwa mwaka 2019 na 2020 jijini Dar es Salaam na baadae mkoani Tanga mwaka 2021.

“Tuna shule nyingi ambazo Serikali imeweka alama maalum lakini wengine hawazifahamu na wengine hawaoni umuhimu wa kuzitumia, kwahiyo kupitia mradhi huu tutawaelimisha,” amesema Kalolo huku akisisitiza ni muhimu kwa jamii ya Watanzania kushirikiana kikamilifu katika kuchukua hatua madhubuti kukomesha ajali za barabarani.
Mkurugenzi wa Shirika la AMEND nchini Tanzania Simon Kalolo akionesha cheti cha ushirikiano bora wa Usalama Barabarani baada ya kumkabidhiwa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news