Polisi Tanzania yajuta kukutana na KMC FC

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KIKOSI cha KMC FC jana kimeanza vema mzunguko wa Pili wa Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa magoli matatu kwa sifuri dhidi ya Polisi Tanzania, mchezo uliopigwa katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi jijini Dar es Salaam.
Magoli hayo ya ushindi kwa KMC FC yamefungwa na Iddi Kipagwile, Emmanuel Mvuyekule pamoja na Sadala Lipangile na hivyo kufikisha jumla ya alama 22 na kupanda kwenye nafasi ya sita mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kutoka nafasi ya 11 iliyokuwa awali kabla ya mchezo huo wa jana.

Katika mchezo huo ambao ulipigwa saa moja jioni, ulikuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo mbili pindi zinapokutana kuwa na ushindani mkubwa tangu zilivyopanda kushiriki michuano ya Ligi Kuu soka Tanzania huku Polisi Tanzania ikipata matokeo zaidi dhidi ya KMC FC.
Afisa Habari na Mawasiliano wa KMC FC, Bi.Christina Mwagala amesema kuwa, timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana imekuwa na muendelezo mzuri wa kupata matokeo ikiwa ni mkakati wa viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji kuhakikisha kwamba inafanya vizuri kwenye kila mchezo na hivyo kuendelea kutafuta nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
"Aidha, matokeo ya mchezo huo wa jana yametokana na ubora wa wachezaji benchi la ufundi ikiwa ni muendelezo mzuri wa KMC kupata matokeo ya kushida mechi mfululizo ambapo kwenye mchezo wa kufunga mzunguko iliibuka na ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Dodoma Jiji na jitihada hizo zitaendelea ili kufikia malengo ya klabu iliyojiwekea,"amesema Bi.Mwagala.
"Tumeanza vizuri mzunguko wa pili, hizi nijitihada kubwa ambazo wachezaji wetu wanafanya wakiwa kwenye mazoezi, lakini pia kufuata maelekezo ya mwalimu anayoyatoa, tunahitaji kuendeleza ubora huu kwa kila mechi ambayo tutacheza, hivyo kikubwa tunazidi kumuomba Mungu awape Afya njema wachezaji wetu kila siku,"ameongeza.

Ameongeza kuwa, kwenye mzunguko wa kwanza hawakuanza vizuri, "na tulipoteza dhidi ya Polisi Tanzania kule Karatu, kwa hiyo kwenye mzunguko huu tuliweka nia kabisa kwamba hatuhitaji kupoteza tena,wachezaji walijituma zaidi na mwisho wa siku tukapata matokeo, hilo ni jambo jema tunawapongeza zaidi wachezaji kwa kazi kubwa wanayoifanya.
"KMC FC kesho itaanza tena maandalizi ya mchezo mwingine dhidi ya Coast Union utakaopigwa siku ya Jumapili ya Machi saba hapa jijini Dar es Salaam na uongozi umetoa mapumziko leo Jumapili na kesho Jumatatu asubuhi programu ya mazoezi itaanza kama ambavyo kocha Mkuu Hitimana ameandaa,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news