Mwalimu Abubakar Allawi aliwezesha vifaa vya ujenzi tawi la CCM Mailimoja

NA ROTARY HAULE

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mdau wa maendeleo kutoka Kibaha Mjini, Abubakar Allawi amelipiga jeki tawi la CCM la Mailimoja lililopo Kata ya Mailimoja kwa kutoa msaada wa mabati 40 pamoja na vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya milioni tatu.
Allawi ametoa msaada huo leo mbele ya kamati ya Siasa ya tawi hilo ikiwa ni sehemu ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa choo cha tawi hilo ambalo kwa muda mrefu walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa choo.

Akikabidhi msaada huo leo kwa niaba ya Mwalimu Allawi mwenyekiti wa kamati ya ujenzi kutoka taasisi ya Allawi Foundation, Mshamu Mbalamwezi amesema kuwa, Allawi ametoa msaada huo baada ya kupata barua ya maombi kutoka katika tawi hilo.

Mshamu amesema, Allawi alipokea barua hiyo wiki tatu zilizopita ikieleza juu ya maombi ya kukamilisha hatua ya upauaji wa choo hicho na kwamba aliona ni vyema akatekeleza ombi hilo kwa haraka.

Amesema,Mwalimu Allawi amekuwa akitoa huduma za aina mbalimbali kwa jamii kupitia taasisi yake ya Allawi Foundation na kwamba huduma anazotoa zinaelekezwa kwa jamii moja kwa moja bila ya ukaguzi.

"Leo Mwalimu Allawi kupitia taasisi yake ya Allawi Foundation tumekuja hapa katika tawi la CCM Mailimoja kwa ajili ya kuleta Bati,Mbao , Misumari na vifaa vingine vya ujenzi kwa ajili ya kusaidia kupaua mradi wa choo cha chama na lengo hasa ni kusaidia jamii,"amesema Mshamu.
Aidha,Mshamu ameongeza kuwa Allawi Foundation imejikita katika kusaidia jamii ambapo mbali na kusaidia chama lakini pia wapo katika kusaidia misikitini, makanisani na hata jamii nyingine yenye mahitaji maalum.

"Tunawaomba wananchi wa Kibaha Mjini na maeneo mengine waitumie taasisi ya Allawi Foundation kutatua changamoto zinazowakabili kwakuwa taasisi yetu imejikita katika kusaidia jamii bila ubaguzi wa dini,kabila na chama," ameongeza Mbalamwezi.

Kwa upande wake Katibu wa CCM tawi la Mailimoja, Shamimu Masoud, amemshukuru Mwalimu Allawi kwa hatua kubwa ya kujitokeza kusaidia utekelezaji wa mradi huo.
Masoud amesema kuwa, waliandika barua nyingi na kuzipeleka kwa wadau , viongozi wa Chama na wafanyabiashara juu ya maombi ya kusaidiwa kukamilisha ujenzi wa choo hicho lakini Mwalimu Allawi amekuwa wa kwanza kujitokeza.

Masoud ameongeza kuwa awali walipata fedha kutoka CCM ngazi za juu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo na kufanikiwa kufikia hatua ya rinta lakini walikwama kuendelea kutokana na fedha hizo kumalizika.

"Baada ya fedha kumalizika kamati ya Siasa ililazimika kufanya maamuzi ya kuwaomba wadau juu ya kukamilisha mradi huu wa choo lakini tunamshukuru Mwalimu Allawi kwa kutufungulia mlango na leo tumepokea Bati,Mbao na vifaa vingine vya ujenzi lakini kikubwa zaidi hata fundi wa kupaua anamlipa yeye,"amesema Masoud.

Masoud amesema, kukamilika kwa mradi huo kunategemea nguvu ya wadau , viongozi wa Chama na hata wafanyabiashara na kwamba amewaomba wadau wengine waliopewa barua na wale wasiopewa barua kuendelea kujitokeza ili kuweza kukamilisha ujenzi wa choo hicho.
"Mradi huu ndio kwanza upo hatua ya upauaji na bado kuna mahitaji mengi yanahitajika ikiwemo madirisha,plasta,vigae (tiles),milango na vifaa vingine hivyo tunaomba wajitokeze zaidi kwakuwa hatua hiyo italeta heshima kwa chama kuwa na choo ambacho kitasaidia utunzaji wa mazingira,"ameongeza Masoud.

Nae mjumbe wa kamati ya siasa wa tawi hilo, Hamisi Mtupa,ameeleza kufurahishwa na kitendo kilichofanywa na Mwalimu Allawi na kusema kuwa huo ni mfano wa kuigwa.

Hata hivyo,Mtupa amesema hatua ya kuchangia ujenzi huo kimelenga kuimarisha chama na wanachama na kwamba atahakikisha vifaa hivyo vinasimamiwa ipasavyo kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news