Radi yawashukia waumini 16 wakiwa wanafanya kazi shamba la Kanisa la KKKT

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAUMINI 16 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Kijiji cha Katani Kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamepigwa na radi huku nane kati yao wakijeruhiwa wakiwa wanafanya kazi kwenye shamba la kanisa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa,William Mwampaghale amethibitisha kutokea kwa tukio hill katika Kijiji cha Katani wilayani Nkasi.
"Tukio hilo lilisababisha taharuki kubwa japo hakuna vifo vilivyoripotiwa, lakini watu nane walipoteza fahamu. Wote 16 walikimbizwa katika Kituo cha Afya Chala kwa matibabu huku hali zao zikielezwa kuimarika,"amesema Kamanda huyo.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Kijiji cha Katani, Jofrey Kisato amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa nane mchana shambani wakiwa kwenye mapumziko huku wakila chakula. 

Amesema kuwa, wakati wakiendelea kula chakula ghafla hali ya hewa ilibadilika ya mvua kutaka kunyesha ndipo ilipopiga radi na kuleta taharuki. 

Alidai kuwa baada ya radi hiyo kupiga wote 16 walizimia na baadae walizinduka huku wanane kati yao hali zao zikiwa mbaya. 

Mwenyekiti huyo wa kijiji alifafanua kuwa wale wanane walikimbizwa katika zahanati ya kijiji hicho na baada ya kupata nafuu wote 16 walipelekwa Hospital ya Kristo Mfalme kwa uchunguzi zaidi.

Kwa nyakati tofauti, wanakijiji wa kijiji hicho wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, huu ni wakati wa kila mmoja kuomba kwa Mungu atoe rehema na uponyaji kwani,matukio ya namna hiyo yamezidi kushika kasi mkoani hapa.

Post a Comment

0 Comments