Rais Dkt.Mwinyi ataja sababu za Serikali kupunguza kodi katika sukari, asisitiza mambo mazuri yanatekelezwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi wote

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya maamuzi ya makusudi ya kupunguza kodi ya sukari ili kuondoa gharama ya bidhaa hiyo katika soko ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi wa Unguja na Pemba.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Februari 28,2022 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Wahariri pamoja na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kukutana nao kila ifikapo mwisho wa mwezi.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa na Serikali ili kupunguza mfumko wa bei hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesema kuwa, hapo siku za nyuma sukari ilikuwa ikitozwa asilimia ya 15 kodi ya ongezeko la thamani ya bidhaa (VAT) na asilimia 25 kodi ya ushuru wa forodha (Import duties) ambapo kwa hivi sasa itatozwa asilimia 12.5 tu kati ya asilimia 25 ili kupunguza gharama katika soko, na kutoa wito kwa wafanyabiashara kuona nia njema ya Serikali katika kuwasaidia wananchi Unguja na Pemba.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo kuona umuhimu wa kutopandisha bei ya vyakula hapa Unguja na Pemba na kusema kuwa sukari imewekewa bei elekezi isizidi 1900 kwa Unguja na 2000 kwa Pemba tofauti ambayo inatokana na usafiri wa Unguja kwenda Pemba.

Hivyo, ameitaka Tume ya Ushindani kutimiza wajibu wake kwa kupita kila duka kuhakikisha bei elekezi zinasimamiwa na watendaji wake wasipofanya kazi hiyo inavyotakiwa basi Serikali itachukua hatua dhidi yao kwani wamepewa jukumu kisheria la kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuzuia mfumuko wa bei usiokuwa na sababu.

Rais Dkt. Mwinyi pia ameeleza azma ya Serikali ya kutumia vifaa vya kukusanya ushuru na kueleza madhumuni ya kutumia mfumo huo na kuwasihi wafanyabiashara kutodharau mfumo huo na kueleza kwamba utaratibu utafanywa ili wafanyabiashara kulipia vifaa hivyo kwa awamu.

Amesema, hatua zitakazochukuliwa katika kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao hususani mara baada ya kumaliza ujenzi wa masoko unaoendelea.

Pia, ameeleza utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha za UVIKO-19, na kusema kwamba miradi ya afya, elimu na maji, umeme na uwezeshaji kazi zinakwenda na huo ndio ujenzi wa nchi.

Amesisitiza usafi wa mji sambamba na kujiandaa na mvua za masika zinazotarajiwa kunyesha, na kuzitaka halmashauri kusafisha na kufanya usafi na kutosubiri mafuriko na Mkurugenzi yoyote ambaye hatowajibika basi atawajibishwa na Serikali.

Akieleza mafanaikio ya mfumo wa Sema Na Rais (SNR), Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kwa asilimia 73 mfumo huo umeweza kupunguza malalamiko na changamoto zinazojitokeza katika jamii na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuutumia mfumo huo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Rais Dkt. Mwinyi alieleza haja kwa wizara husika kuangalia suala zima la Sheria ya Habari kwa vile imepitwa na wakati sambamba na kulitolea maelezo suala la shamba la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililooo Makurunge huko Bagamoyo, Tanzania Bara.

Pia, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza mishahara na kulipa posho zote za wafanyakazi wa Serikali pale makusanyo yatakapoimarika.

Ameeleza haja ya redio za kijamii kuhakikisha nazo zinafaidika na matangazo huku Idara husika ya Elimu kuhakikisha inaondosha usumbufu kwa wanafunzi katika kuwapatia stakabadhi zao kwa kuwapelekea shuleni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news