Rais Samia akoleza kasi ya kumtua mama ndoo kichwani, aweka jiwe la msingi mradi wa maji wa kihistoria mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Safi wa Mugango-Kiabakari- Butiama unaotekelezwa Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara ambapo utagharimu shilingi Bilioni 70.5 na utanufaisha vijiji zaidi ya 39 vyenye wakazi wapatao 165,000.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akicheza ngoma ya Singeli pamoja na viongozi mbalimbali na wananchi wa Kijiji cha Mugango Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuweka jiwe la Msingi Mradi wa Maji Safi wa Mugango,Kiabakari,Butiama leo Februari 6, 2022, Mhe. Rais Samia yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku nne ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi. (Picha na Ikulu).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiondoa kitambaa kama ishara kuweka jiwe la Msingi Mradi wa Maji Safi wa Mugango,Kiabakari,Butiama katika Kijiji cha Mugango Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara leo Februari 6, 2022. (Picha na Ikulu).

Rais Samia ameweka jiwe hilo la msingi leo Februari 6, 2022 ambapo amesema kuwa, dhamira ya Serikali ni kupeleka huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ili kumtua mwanamke ndoo,hivyo dhamira ya Serikali ni kuona inatekelezwa kama ulivyopangwa ili Desemba, 2022 uanze kuwanufaisha wananchi. 

Rais Samia ameitaka serikali ya Mkoa wa Mara na Wilaya ya Musoma kusimamia kidete mradi huo ukamilike kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Butiama na Musoma. Huku akisema jumla ya fedha zilizoletwa upande wa elimu na afya ni Bilioni 3.4 na upande wa TARURA Bilioni 25.4.
Aidha, Mheshimiwa Samia amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendeleza ujenzi wa miradi mikubwa na ya kimkakati na amewatoa shaka wananchi waliodhani miradi haitatekelezeka, wajue kwamba miradi inajengwa kwa kasi kuliko awali.

Aidha, Mheshimiwa Samia amesema kuwa Mkoa wa Mara kuna tatizo la miradi kusuasua na kwamba suluhisho la jambo hilo analifanyia kazi kuimarisha ufanisi wa miradi kwa manufaa ya wananchi. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema kuwa mradi huo utazalisha lita milioni 35 ambapo umeanza kujengwa 17/12/2020 na utakamilika Desemba 17, 2022 ukijengwa na Kampuni kutoka nchini Lesotho na kwa sasa umefikia asilimia 38 na bomba lililoingia Ziwa Victoria ni mita 270 ambapo ukimalizika utatatua changamoto ya maji na kuchochea maendeleo kwa wananchi. 
Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso amesema Wizara hiyo itafanya kazi mchana na usiku kumaliza changamoto ya maji mijini na vijini hapa nchini. Huku akisema Mkandarasi aliyekuwa akijenga awali mradi huo alifukuzwa kutokana na kushindwa kuutekeleza kwa ufanisi na kwa sasa utatekelezeka kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Aweso ameongeza kuwa, awali fedha za miradi ya maji zilichezewa sana kwa kuliwa ambapo ilikuwepo miradi kichefuchefu ipatayo 177, ambapo kwa sasa miradi 126 kupitia RUWASA imepanuliwa na inatoa huduma kwa wananchi maeneo mbalimbali nchini.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo amesema ujenzi wa mradi huo ni mwarobaini tosha wa kumaliza tatizo la maji ambapo amewaomba wananchi kutumia maji hayo kwa shughuli za umwagiliaji kilimo cha mahindi, dengu, ambapo vijiji vya Jimbo la Musoma Vijijini kwa asilimia kubwa vitanufaika na mradi huo. Huku akiwataka Wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo uweze kuleta manufaa kwao. 

Aidha, Prof.Muhongo amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia utoaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Musoma Mjini kwenda Busekera Wilaya ya Musoma Vijijini yenye urefu wa kilomita 92 kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumamne Sagini amesema kuwa, mradi huo ni ushahidi tosha kuwa Serikali ya chama hicho inatenda kwa vitendo. Ambapo wakati wa kampeni amesema aliulizwa na wananchi kuhusu kukwama kwa mradi huo,lakini kwa sasa wananchi wanapongeza na kufurahi kwa moyo mkunjufu.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Happi amesema kuwa, tangu Mheshimiwa Samia ameingia madarakani jumla ya fedha za maendeleo zilizoletwa ni Shilingi zaidi ya Bilioni 126 ambapo miradi ya maji mbalimbali inayekelezwa ukiwemo ujenzi wa chujio la maji Mugumu katika Wilaya ya Serengeti kwa Shilingi Bilioni 1.2, mradi wa maji Rorya unaogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 400, huku Mitaa 9 ya Manispaa ya Musoma ambayo haikuwa na maji kwa sasa itakuwa na maji kutokana na fedha za UVIKO-19 kuwezesha mitaa hiyo kupata maji.

Mheshimiwa Happi ameongeza kuwa, jumla ya Shilingi Bil.4.5 zimetolewa katika Majimbo yote ya Mkoa wa Mara ambazo zitatekeleza mradi wa maji katika kuhakikisha changamoto ya maji inakwisha. 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Christina Mdeme amesema kuwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa kwa ufanisi kutokana na miradi mbalimbali mikubwa na yenye manufaa kwa wananchi kuendelea kutekelezwa ukiwemo mradi huo wa maji ambao utamtua mama ndoo kichwani.

Aidha, Mdeme amewataka wananchi kutunza mradi huo kusudi usaidie vizazi na vizazi na pia akawasisitiza Watanzania wote kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi za kuleta Maendeleo kwa Watanzania. 

Mheshimiwa Innocent Bashungwa ni Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) amesema kuwa, Rais Samia ametoa Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 618 katika Mkoa wa Mara, Shilingi Bilioni 11.9 kwa ajili ya kutekeleza sera ya elimu bila malipo, fedha za ujenzi wa Vituo vya afya 10, ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule shikizi 90.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mashimba Ndaki amesema Wilaya ya Musoma imepiga hatua katika kuachana na vitendo vya uvuvi haramu vilivyokuwa vimeshamiri ambapo amewataka wavuvi kujiunga kwenye vikundi wapewe boti za uvuvi kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news