SERIKALI KUGHARAMIA MATIBABU YA PROFESA JAY ANAYETIBIWA MUHIMBILI

NA SOPHIA MTAKASIMBA-MNH

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu aliyekuwa Mbunge wa Mikumi na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Bw. Joseph Haule (Prof. Jay) anayetibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hadi hapo atakaporuhusiwa kwenda nyumbani.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipofika kumjulia hali msanii huyo na kuwasilisha salamu za Mhe. Rais.

“Nimefika kuleta salamu za Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo safarini nje ya nchi, amesema kuwa anatambua mchango wa Prof. Jay akiwa Mbunge wa Mikumi lakini pia kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia muziki hivyo kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu yake hadi hapo ataporuhusiwa kutoka hospitalini na ninauagiza Uongozi wa Hospitali kuleta bili zote Wizarani kuanzia sasa,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema Mhe. Rais anatoa pole za kuuguza kwa familia ya Prof. Jay na pia anamtakia kila la heri katika matibabu anayoendelea nayo, apone haraka ili aendelee na shughuli zake.

Kwa upande wake mke wa Prof. Jay, Bi. Grace Mgonjo amemshukuru Mhe. Rais na kusema kuwa amefanya jambo kubwa sana kwa familia yake na kuongeza kuwa hawajajuta kufuata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili. 

“Naushukuru sana Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa tangu tulipofika hapa, walitupokea vizuri sana na hatujawahi kujutia kuwa hapa,” amesema Bi. Grace.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amemuhakikishia Waziri Ummy kuwa amepokea maelekezo na atayatekeleza vizuri. 

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kazi kubwa wanayoifanya katika utoaji wa matibabu ya kibingwa yanayotolewa kwa Watanzania na kuahidi kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika kufanya kazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news