Polisi wataja mbinu zilizotumika kuiba Bilioni 2.13/- za Selcom, Kileo atoa rai

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Iringa linafanya uchunguzi dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa fedha za kitanzania kiasi cha shilingi bilioni 2,129,856,000 mali ya Kampuni ya SELCOM PAYTECH LIMITED.
Hayo yamebainishwa leo Februari 11, 2022 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, wakati akielezea kuhusiana na tukio hilo ambalo linatajwa kuwa la aina yake nchini. 

Kamanda huyo amesema kuwa, Wakala wa Selcom aitwaye Tyson Kasisi wa Iringa kupitia huduma ya Selcom Pay isivyo halali alihamisha fedha kwenda namba mbalimbali za simu na kisha kuchukuliwa taslimu kupitia wakala wa huduma za kifedha za mitandao mbalimbali ya simu pamoja na akaunti za benki.

“Wizi wa fedha hizo ulifanyika kwa njia ya mtandao katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, Dar es Salaam na Morogoro kati ya tarehe 9 hadi 27 Novemba, 2021 baada ya wakala huyo Kasisi kufanikiwa kuchezea mfumo wa kieletroniki wa Selcom Pay unaomilikiwa na Kampuni ya SELCOM PAYTECH LTD.

“Wakala huyo kwa njia ya udanganyifu alianza kujitumia fedha pamoja na kuwatumia watu wengine na kwa kushirikiana na genge lake la uhalifu walifanikiwa kuiba kiasi hicho, Jeshi la Polisi Iringa limefanikiwa kukamata fedha taslimu kiasi cha sh. 956,974,000 kutoka kwa watuhumiwa na washiriki wa uhalifu huo ambao walipokea sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kuzificha katika maeneo mbalimbali ikiwemo makazi na shambani,"amefafanua Kamanda huyo.Mbali na Tyson Kasisi wanufaika wakuu wa uhalifu huo wametajwa kuwa ni Patrick Chalamila na Evaristo Chalamila.

"Mali ambazo ni mazalia ya uhalifu zimekamatwa na kuhifadhiwa ikiwa ni magari manne yenye thamani ya sh. 303,000,000 ambayo ni Scania yenye jina la mtuhumiwa Patric Chalamila kwa thamani ya sh. 128, 000,000, Mitsubishi Fuso yenye jina la Tyson Kasisi kwa thamani ya sh. 75,000,000 na Toyota Harrier yenye jina la Tyson Kasisi kwa thamani ya sh. 72,000,000, Nissan Juke yenye jina la Patrick Chalamika kwa thamani ya sh. 28,000,000.

"Pia tumekamatwa gari Toyota IST mali ya Patrick Chalamila, lililotumika kufanikisha uhalifu kwa kusafirisha fedha za wizi kutoka Madibira wilayani Mbarali na Ilula wilayani Kilolo kwenda kuzificha Kilombero mkoani Morogoro. Ushahidi uliokusanywa mpaka sasa umetosha kuwafikisha watuhumiwa 10 mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili kwa makosa ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,"ameongeza Kamnda huyo.

Kileo

Wakati huo huo, Mtaalamu wa Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Digitali nchini, Bw. Yusuph Kileo amesema ili kushinda uhalifu mtandao, wahanga wanapaswa kutoa taarifa mara moja ili hatua za haraka zichukuliwe.

"Nimekuwa nikihamasisha sana wahanga wa uhalifu mtandao kutoa taarifa mara moja, hatua zichukuliwe.Nimepata maoni mengi kuwa kumekuwa na hamasa ndogo ya kuripoti matukio ya kihalifu mtandao kutokana na wanaotoa ripoti hawaoni kinachoendelea.Aidha, Bungeni nimesikia mbunge akilalamikia hili pia.

"Natoa wito makosa ya kimtandao yanaporipotiwa, hatua za haraka zichukuliwe.Hii itaongeza imani kwa watu kuwa, matatizo haya yanafanyiwa kazi na itaondoa mwanya kwa mhalifu kupoteza ushahidi au kupotea,"amefafanua Kileo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news