Spika Dkt.Tulia Ackson afunguka kuhusu wabunge 19 wa CHADEMA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Ackson amesema wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliopo bungeni wapo kihalali.
Wabunge hao ni Halima Mdee,Asia Mohamed, Felista Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Simon, Anatropia Theonest,Salome Makamba, Conchester Lwamraza, Grace Tendega, Ester Matiko,Secilia Pareso,Ester Bulaya, Agnes Kaiza, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Tunza Malapo.

Ingawa amesema anasubiri michakato halali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ngazi zingine na iwapo itathibitika hakuna shida atatekekeza takwa la kikatiba.

Mheshimiwa Spika Dkt.Tulia ametoa kauli hiyo leo Februari 14, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na wahariri na waandishi mbalimbali wa habari wanaoripoti habari za Bunge.

Akijibu swali kuhusu uhalali wa wabunge wao, Spika amesema hadi sasa wabunge hao wapo kwa mujibu wa sheria, kwani kila mbunge ni lazima atokane na chama na hao nao wametokana na chama.

Pia amesema, Bunge halioni shida kuwaondoa wabunge na lilishawahi kufanya hivyo katika mabunge yaliyotangulia huku akibainisha kuwa, mchakato wa namna gani walifika bungeni si hoja ambayo Bunge linatakiwa kujibu bali wenye majibu ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mheshimiwa Dkt.Tulia amesema taarifa itakayopelekwa bungeni kuhusiana na wabunge hao sharti iwe imekidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kwa kutendewa haki na yeye hatakuwa na shida kwenye maamuzi.

Novemba 2020 waliapishwa wabunge 19 wa Chadema ambao walizusha malumbano ya namna waliteuliwa na majina yao kupelekwa Bungeni kwani chama chao hakikutoa ridhaa.

Kilichojiri

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, mwezi Novemba 2020 alisema Kamati Kuu ya Chama hicho iliyoketi Novemba 27,2020 iliazimia kuwavua uanachama Halima Mdee na wenzake 18 waliopishwa juzi kuwa Wabunge Viti Maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mbowe alisema wabunge hao walikinajisi chama na walikataa kwenda kwenye Kamati Kuu kuhojiwa.

“Pia Kamati Kuu imewavua uongozi wale wote ambao walikuwa viongozi kwenye mabaraza kati ya hao dada zetu 19 sitaki kupoteza muda kuwataja majina, kwa hiyo kuanzia sasa hawapaswi kushughulika na lolote kama viongozi na tumeelekeza nafasi zao zizibwe haraka,”alisema Mbowe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news