Tiba migogoro mali za marehemu yatajwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MIGOGORO ya kugombania mali ndani ya familia huanza pindi anapofariki mmiliki mmoja wa mali zilizopo,na mgogogoro hutokea pindi marehemu hakuacha wosia wowote juu ya mali zilizopo,aina ya mali zimilikiwe na nani na kwa utaratibu gani. 

Jamii nyingi zmekuwa zikiishi maisha ya mazoea bila kuona umuhimu wa kuweka mali zake katika utaratibu ili kuepuka migogoro pindi atapofariki na kuacha watoto na ndugu zake wakigombana,wakipigana na wengine kuuana juu ya mali ambazo hawakuchuma. 
Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakiwa katika kikao cha mwezi cha kujadilia utendaji wao wa kazi ikiwemo changamoto wanazokutokana nazo ndani ya jamii. (Na Mpigapicha Wetu).

Tukumbuke kuwa wosia ni kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake kuonesha nia yake jinsi gani angependa mali zake zigawanywe baada ya kufa kwake,unaweza kuwa wa maandishi na sio wa maandishi.

Sheria inaweka bayana kwamba kuandikisha wosia sio lazima,bali ni hiari ya muhusika,wosia wa mdomo hauwezi kufuta au kubadilisha wosia wa maandishi,lakini wosia wa maandishi waweza kufuta au kubadilisha wosia wa mdomo ikiwa mashahidi wa wosia wa mdomo watashiriki. 

Utamaduni wa kutojua sheria ya wosia na mirathi inapelekea jamii nyingi kuwa na mgogoro mara kwa mara,pia kufungua kesi zisizoisha mahakamani,na hii inapelekea kutumia gharama na muda mrefu kupigania mali ambazo hawakuzitafuta ila wanapaswa kuzipata kwa utaratibu uliopo. 

Pia inatupasa kujua sheria za urithi zenye kugawa mali sawa bila ubaguzi wowote,kwani warithi wa marehemu sheria inawatambua na inaeleza namna ya kugawa mali zilizoachwa na marehemu,na sheria imewekwa wazi ili itoe muongozo wa kugawa mali za urithi. 

Sheria zinazohusu urithi na wosia Tanzania zimegawanyika katika sheria za aina tatu,ambazo ni sheria ya serikali,sheria ya mila na sheria dini ya kiislam,wanafamilia katika kugawa mali alizoacha ndugu yao wanaweza kutumia sheria mojawapo kugawa mali ili kuepuka mgogoro ndani ya familia. 

Familia nyingi zimeonekana kugawa mali zilizoachwa na ndugu zao kwa kutofuata sheria na taratibu zilizowekwa na hatimaye kuingia kwenye mgogoro,na sheria hizi zinakubali uwepo wa wosia alioacha marehemu wakati wa uhai wake ambao unaonyesha utaratibu wa mali zake alizochuma. 

Tunaamini wosia ukiwepo unarahisisha ugawaji wa mirathi kwani matakwa ya marehemu ndiyo yatakayozingatiwa,na kuwepo kwa wosia uliozingatia vipengele vya sheria husaidia kupunguza matatizo na kutoelewana miongoni mwa warithi au ndugu juu ya mali iliyoachwa na marehemu. 

Shabani Kimwaga anasema katika eneo la Mngazi Halmashauri ya Morogoro jamii nyingi bado hazifuati mfumo wa sheria katika kugawa mali zilizoachwa na ndugu zao baada ya kufariki,na hii imechangia ndugu wanaobaki kujenga chuki na wengine kufikia hatua ya kuuana. 

“Kuna baadhi familia baba akifariki ndugu wa familia humfukuza mke wake(mjane),na kumwambia hawezi kuishi ndani ya familia hiyo kutokana na mme wake hayupo,na baadhi ya mali wanarithi hao na yeye kupewa mali kidogo sana,”anasema Shabani.

Anasema hali hii inatokana ukosefu wa elimu,kutojua sheria na hivyo kupelekea kufanya maamuzi yasiyo sahihi ambayo yanasababisha vurugu na matengano ndani ya familia na wengine wanafikishana mahakamani. 

Anaongeza kuwa, watu wanaoishi pembezoni mwa mji ndio wahanga wakuu wa katika kesi za mirathi na wosia,wamekua wakiishi bila kufuata sheria na wengine wanaamini katika mila na desturi ambazo kwa asilimia kubwa ni kandamizi kwa wanawake. 

Kila jambo huwa na faida na hasara yake kulingana na vile linavyotumika, na ndio maana siku watu hufanya jambo au hutenda fulani kutokana na faida zake na sio hasara zake, wosia unapokuwepo una kuwa na faida kubwa kwa familia pia kwa vyombo vya sheria kuweza kutenda haki. 

Tukumbuke kuwa mtu atakapoacha wosia ugomvi usio kuwa na mantiki au malengo hautotokea kwani mgawanyo wa mali utakuwa umeoneshwa, pia ugomvi wa marehemu atazikwa alipofia ama asafirishwe au asisafirishwe yote yatakuwa yameondolewa kama marehemu aliacha wosia unaoelezea kila kitu kumuhusu yeye. 

“Wosia ni chanzo cha kuondosha migogoro yoyote inayojitokeza ndani ya familia,tujifunze na kuelewa umuhimu wa kuacha wosia wakati tukiwa hai,tuachane na mila potofu na maneno yanayosemwa ukiandika wosia unajiombea mauti mapema,”amesema. 

Wosia ndio nyenzo pekee ambayo inaweza kufichua vitu ambavyo vilikuwa havijulikani juu ya marehemu husika, mfano marehemu aliacha mali ngapi au marehemu anadaiwa na kampuni fulani au anawadai watu wangapi, ambavyo ndugu walikuwa hawavifahamu, hivyo wosia utakuwa chanzo cha kuweka bayana mambo yote yaliyojificha juu ya marehemu. 

Pia wosia utaonyesha wanufaika wengine wa mali za marehemu ambao sio ndugu wa damu,hi ni pale marehemu alipoandika wosia kuwa moja ya tatu ya mali zangu wapewe watu fulan kama vile mayatima au iwe msikitini au kanisani. 

Katika wosia ndugu wa marehemu wanapswa kuujua na kuutumia kugawa mali kama marehemu alivyosema katika wosia wake juu ya mali yake, na wengine ambao sio ndugu wa damu wataweza kunufaika kwa mali hiyo ya marehemu baada ya mgawanyo wa mali kufanyika chini ya msimamizi wa mirathi. 

Aidha wosia hutoa maelekezo nini cha kufanya baada ya yeye mwandika wosia kufariki dunia,kama kimfano vipi azikwe au mwili wake uwe zawadi kwa wale wanaojifunzaa mambo ya kisayansi au maelekezo mengineyo juu ya kile anachokitaka kifanyike katika mali zake baada ya yeye kufariki dunia.

Msaidizi wa Kisheria kutoka Wilaya ya Mvomero,Gabriel Ngoi anasema bado kuna nafasi kubwa ya wadau wa maendeleo na serikali kuendelea kutoa elimu ndani ya jamii lengo la kuhakikisha kesi za mirathi zinaisha hazitokei katika jamii. 

Ngoi anasema wasaidizi wa kisheria wanafanya kazi kubwa ndani ya jamii ya kutoa elimu katika mirathi na wosia na katika nyanja nyingine ikiwemo ukatili wa kijinsia,hii imewajenga wananchi kujua nini cha kufanya kuondokana na changamoto inayowakabili. 

“Mashauri ya mirathi yanapotufikia tunayafanyia kazi kwa kufuata muongozo wa sheria,na mashauri yanayotufikia ni unakuta hawana wosia,na hiyo ndio inachangia kuweza kufika katika vyombovya sheria kuomba msaada,bado tunasisitiza wananchi watambue wosia ni jambo muhimu na linapaswa kupewa kipao mbele”Anasema Ngoi. 

Aidha, katika kuhakikisha dhana ya wosia inakua kwa mapana,kunatakiwa kuwepo mashirikiano ya wadau kwa pamoja,ikiwemo viongozi wa dini kutumia majukwaa kutoa elimu,viongozi wa serikali na siasa kutumia nafasi zao kuhubiri ili kuweza kutokomeza migogoro inayotokana na wosia na mirathi. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news