Waziri Mhagama:Wajibu wa watumishi wa umma ni kufanya kazi kwa bidii

NA MWANDISHI MAALUM-PSC

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Jenista J. Mhagama (Mb) amesema wajibu wa Watumishi wa Umma ni kumuunga mkono Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa bidii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Jenista J. Mhagama (Mb) akizungumza na Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma, katika Ofisi ya Tume Chimwaga Dodoma, mwishoni mwa wiki, wa kwanza kulia ni Bw. Mathew M. Kirama, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma. (Picha na PSC).

Mheshimiwa Mhagama amesema haya mwishoni mwa wiki wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, uliofanyika Jijini Dodoma.

“Wajibu wetu Wafanyakazi ni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajibika ipasavyo, kufanya kazi kwa weledi, bidii, uaminifu mkubwa na kutoa huduma bora kwa wananchi tunaowahudumia. Kuwahi kazini na kutekeleza majukumu yetu huku tukiangalia malengo tuliyojiwekea yanafikiwa ni jambo la muhimu sana. Msishushe viwango vya utendaji kazi ni lazima mhakikishe mnakwenda viwango vya juu. Ni muhimu sana kila Mtanzania akawajibika na mtumishi wa umma akiwajibika kikamilifu ni lazima apate haki yake,” alisema Waziri Mhagama.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama (wa kwanza kulia) akisisitiza mshikamano kwa watumishi wa Tume, kulia kwake ni Mheshimiwa Jenista J. Mhagama (Mb) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, hii ilikuwa katika Ofisi ya Tume Chimwaga Dodoma. (Picha na PSC).

Akizungumzia kuhusu majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Mhagama alisema Tume imepewa jukumu kubwa la urekebu wa Utumishi wa Umma nchini, kuhakikisha Utumishi wa umma unasimamiwa na unaendeshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo halali yanayotolewa na Serikali.

“Tume hii ni chombo chenye majukumu mazito na nyeti ya kusimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma fanyeni kazi kwa bidii, muongozwe na uzalendo kwa maslahi ya Watanzania huku mkipambana na rushwa, ufisadi au aina nyingine yoyote ya uovu unaopingana na Maadili ya Utumishi wa Umma. Tambueni suala la kuitunza Rasilimali Watu ni suala la kipaumbele, ujengwaji wake unachukua muda mrefu lakini kuibomoa ni suala la siku moja na inakuwa ni hasara kwa Serikali na Taifa linaondokewa na nguvu kazi. Hivyo, dhamana mliyopewa ya kuisimamia na kuitunza Rasilimali Watu ni kubwa, hakikisheni Rasilimali Watu hii katika Utumishi wa Umma inatunzwa ipasavyo na inaleta tija katika utendaji wake wa kazi” alisisitiza Mheshimiwa Mhagama.

Akizungumza kuhusu jukumu la Tume la kushughulikia rufaa na malalamiko, Mheshimiwa Waziri Mhagama alisema, Tume imeshika haki na maisha ya wafanyakazi, kwa kuwa ndio inayotoa maamuzi ya rufaa na malalamiko mengi yanayowasilishwa mbele yake kuhusu watumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Jenista J. Mhagama (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma, kulia kwake ni Bw. Mathew M. Kirama Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma. (Picha na PSC).

“Hakikisheni siku zote mnasimama kutenda haki, mhukumu kwa haki lakini kwa wale wanaotaka kuhujumu juhudi za Serikali kwa kufanya ubadhirifu na wamo ndani ya Utumishi wa Umma mkikutana na kesi zao washughulikieni ipasavyo” alisisitiza.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama alimhakikishia Mheshimiwa Waziri Jenista J. Mhagama (Mb) kuwa hakuna haki ya mtumishi wa umma itakayopotea mbele ya Tume lakini pia, hakuna mtumishi wa umma atakayepewa haki asiyostahili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news