WAZIRI WA MADINI WA ZIMBABWE AWASILI DODOMA

NA STEVEN NYAMITI-WM

WAZIRI wa Madini wa nchi ya Zimbabwe, Mhe. Wiston Chitando na ujumbe wake akiambatana na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo Mhe. Prince Machaya wamewasili nchini kwa ziara ya kikazi inayolenga kuzungumzia masuala yanayohusu Umoja wa Nchi zinazozalisha madini ya Almasi (Association of Diamond Producing Countries – ADPA) na Kimberly Processing Certification System (KPCS). 
Kabla ya kuwasili jijini Dodoma, Waziri Chitanda alipokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo na Afisa Madini Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Ally Maganga jijini Dar es Salaam.

Aidha, kutokana na Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Umoja huo kwa sasa, ni fursa kwa Zimbabwe ambayo ni Makamu Mwenyekiti kupata taarifa kuhusu umoja huo ikiwa ni maandalizi ya nchi hiyo kuchukua nafasi ya uenyekiti baada ya Tanzania kumaliza muda wake.
Mbali na kuzungumzia masuala ya umoja huo, pia ujumbe huo unatarajia kukutana na Wakuu wa Taasisi za Wizara na Wataalam wake ambapo watafahamishwa kuhusu masuala muhimu yanayosimamiwa na wizara na baadhi ya taasisi zake ambazo ni Tume ya Madini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Post a Comment

0 Comments