WIZARA YA ARDHI YAKAMILISHA UANDAAJI RAMANI ZA KIDIGITALI KATIKA HALMASHAURI 38

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekamilisha uandaaji ramani za kidijitali zinatotumika kama ramani za msingi kwenye utekelezaji mfumo wa anuani za makazi katika halmashauri 38 nchini.Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete akizungumza katika uzinduzi wa operesheni maalum ya kukamilisha uwekaji anuani za makazi nchini uliofanyika Ukumbi wa Mkutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre Dodoma. (PICHA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM).

Aidha, Wataalamu wa Wizara ya Ardhi wanaendelea kutekeleza kazi ya kubadilisha ramani kutoka kwenye mfumo wa analogia kwenda digitali na kutambua maeneo yasiyopimwa, kuandaa ramani za mipaka ya kiuatawala katika halmashauri mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa Februari 8,2022 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete wakati wa uzinduzi wa operesheni maalum ya kukamilisha uwekaji anuani za makazi nchini uliofanyika ukumbi wa mkutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre Dodoma.

Kwa mujibu wa Ridhiwani, Wizara ya Ardhi imejipanga kikamilifu kuhakikisha zoezi la uandaaji ramani za kidigitali linakamilika ndani ya muda ili kuwezesha utoaji anuani za makazi.

‘’Wizara tutanufaika sana na taarifa zinazokusanywa kwenye mfumo wa anuani za makazi kutokana na kutumia taarifa hizo kuhakikisha tunaboresha taarifa zilizopo kwenye mifumo ya usimamizi wa ardhi, kuimarisha ukusanyaji mapato ya ardhi pamoja na kuboresha utoaji huduma za ardhi kwa kutumia anuani za makazi,"amesema.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete (kulia) akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa wakati wa uzinduzi wa operesheni maalum ya kukamilisha uwekaji anuani za makazi nchini uliofanyika ukumbi wa mkutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre Dodoma.(PICHA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM).

Naibu Waziri wa Ardhi aliongeza kwa kusema, zoezi hilo la kubadilisha ramani kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali lilianza katika halmashauri zote tano za mkoa wa Dar es salaama, jiji la Dodoma pamoja na halmashauri nyingine za mikoa ya Tabora, Kagera, Tanga na Mbeya.

‘’Iwapo zoezi hili likifanyika kikamilifu nchi nzima litawezesha Wizara ya Ardhi kuongeza uwezo wa kusimammia uendelezaji miji, utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa njia ya kidigitali kwa kuwa ramani zote za mipango miji na upimaji nchini zitakuwa kwenye mfumo huo zikibainisha viwanja au mashamba matumizi yake,"amesema Ridhiwani.

Alisema, ulinganifu wa kitakwimu utawezesha Wizara ya Ardhi kutoa huduma bora zaidi na kusimamia upatikanaji taarifa za wamiliki wa ardhi kupitia mfumo unganishi wa taarifa za ardhi ILMIS. Pia utarahisisha kutambua maeneo kwa ajili ya uwekezaji, na shughuli mbalimbali kama makazi mashamba na maeneo ya kufugia na shughuli za uchumi.

Hata hivyo, mbali na faida za kitakwimu zinazopatikana kwenye zoezi la anuani za makazi alibainisha kuwa, lengo la uandaaji ramani hizo ni kurahisisha upatikanaji taarifa sahihi za ardhi ambazo ni muhimu katika kujenga msingi wa anuani za makazi pamoja na utekelezaji maono ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha ardhi inapangwa, inapimwa na kurasimishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news